Mbwembwe za kijeshi zatawala mapokezi ya Rais wa China Xi Jinping nchini Marekani



Rais wa Marekani Donald Trump amempokea Rais wa China Xi Jinping kwa heshima kubwa ya zulia jekundu na ndege za kivita zilizopita angani katika Kituo cha Kijeshi cha Andrews wakati alipowasili kwa ziara rasmi ya kihistoria ya siku tatu nchini humo.

Aidha Waziri wa fedha wa Marekani Scott Bessent ametangaza kuwa nchi hizo mbili zimeafiki kuongeza muda wa sitisho la vita vya kibiashara hadi mwezi Januari. 

Katika mapokezi hayo adimu yaliyojumuisha kupigwa kwa mizinga 21, bendi ya kijeshi, na kuwasili kwa viongozi hao pamoja na wake zao, Rais Trump alimsifu mgeni wake kama kiongozi mkuu na kwamba tukio hilo ni la kihistoria, wakati Rais Xi alisema kuwa China na Marekani zinapaswa kuwa washirika badala ya wapinzani na kwamba ustawi wa nchi zote mbili unaweza kwenda sambamba na kufaidisha ulimwengu. 

Hata hivyo, mapokezi hayo ya kifahari yamezua hoja ndani ya chama cha Republican, huku baadhi ya wabunge na wataalamu wa Marekani wakionya kuwa ukaribu wa viongozi hao kunapingana na kanuni za kisiasa za Marekani za kupinga mifumo ya kisoshalisti au kikomunisti duniani.




Katika ziara hiyo ambapo mazungumzo ya faragha na chakula cha jioni cha kitaifa kitafanyika, masuala kama vile ushuru wa bidhaa, teknolojia ya akili unde (AI), vita vya Iran na Taiwan yanatazamiwa kujadiliwa.

Aidha, uamuzi wa kuongeza muda wa sitisho la vita vya kibiashara hadi Januari 10 unatajwa kama hatua nzuri ya awali kabla ya mazungumzo hayo magumu kuanza rasmi.

Ziara hii inafuatia mkutano wao wa hapo awali uliofanyika nchini China mwezi Mei.Licha ya mbwembwe za kijeshi na ahadi kadhaa za kibiashara, wachambuzi wanabainisha kuwa mikutano hiyo mara nyingi huwa na mijadala migumu huku kukiwa na masuala mengi nyeti ya kimataifa yanayohitaji suluhu ya kudumu kati ya nchi hizo mbili zenye nguvu kubwa zaidi za kiuchumi duniani.

No comments