NISHATI YAELEZWA KUWA CHACHU YA KILIMO, UCHUMI NA MAENDELEO YA VIJIJINI




Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy, amesema upatikanaji wa nishati bora umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa kuwezesha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo, ikiwemo umwagiliaji, uchakataji na uhifadhi wa mazao, pamoja na kukuza biashara na viwanda vidogo vijijini.

Amesema kutokana na  upatikanaji wa nishati ya uhakika wananchi wameweza kuongeza tija na kukuza kipato chao huku wakichochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Mkurugenzi huyo alisema hayo wakati akizungumza katika banda la wakala huo kwenye maonesho ya  wakulima ya Nane Nane 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Aidha amewataka wananchi kutembelea banda la wakala huo, ili kujionea mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini na kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala huo. 

Akifafanua zaidi Saidy amesema kuwa REA inaendelea kutekeleza miradi ya umeme vijijini na nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi ili kuchochea shughuli za uzalishaji, kuboresha huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini. 

Aidha, ameeleza kuwa  Mha. Saidy amesisitiza kuwa Banda la REA ni fursa muhimu kwa wananchi na wadau kupata elimu kuhusu utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini, kufahamu mafanikio yaliyopatikana na kuelewa mchango wa nishati katika kuimarisha maendeleo ya wananchi hususan waishio vijijini ili kuitekeleza kivitendo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

No comments