WAKALA WA VIPIMO WAELEZA TIBA YA GESI PUNGUFU
WANANCHI wametakiwa kuhakikisha wanapima mitungi ya gesi kabla ya kuinunua ili kujiridhisha kuwa wanapata kipimo cha gesi kinacholingana na fedha wanazolipa.
Aidha wafanyabiashara wote wa gesi wamekumbushwa kutimiza matakwa ya kisheria ya kuwa na mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA).
Rai hiyo imetolewa na Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Singida, Willie Amosi, wakati wa Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma ambapo amesema matumizi ya gesi ya kupikia yameongezeka kwa kasi kufuatia jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Amesema jukumu la Wakala wa Vipimo ni kuhakikisha kila mtungi wa gesi unaouzwa kwa wananchi unakuwa na kipimo sahihi cha gesi kama kilivyoainishwa na mzalishaji, ili kumlinda mlaji dhidi ya hasara inayoweza kusababishwa na vipimo visivyo sahihi.
"Wananchi wana haki ya kujiridhisha kuwa gesi wanayonunua ina uzito sahihi. Ndiyo maana sheria inamtaka muuzaji wa mwisho kuwa na mizani iliyohakikiwa na WMA ili kila mnunuzi aweze kupima mtungi wake kabla ya kuuchukua," amesema Amosi.
Ameeleza kuwa kila mtungi wa gesi hubeba taarifa zinazoonyesha uzito wa mtungi wenyewe pamoja na kipimo cha gesi kilichomo ndani, hivyo mnunuzi anapaswa kulinganisha taarifa hizo kwa kupima mtungi kwenye mizani iliyothibitishwa.

Post a Comment