KABAILA HAYAWANI YAACHA SIMULIZI DAR

 




WAPENZI wa sanaa wamepata fursa ya kujionea ubunifu wa hali ya juu na mwingiliano wa kitamaduni katika onesho la mchezo wa jukwaani unaoitwa ‘Kabaila Hayawani’ lililofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Sayansi na Utamaduni wa Urusi Dar es Salaam. 

Mchezo huo wa juzi ulitayarishwa na Kituo cha Sayansi na Utamaduni wa Urusi kwa kushirikiana na kundi la African Film Arts and Social Revolution (AFASR) na kuongozwa na Nyakwesi Mujaya. 

Mchezo huo unatokana na hadithi ya mwandishi mashuhuri wa Kirusi, Mikhail Saltykov-Shchedrin na unabeba mafunzo, burudani na tafakuri kuhusu maisha halisi ya kijamii. 

Ofisa Maendeleo ya Filamu wa Bodi ya Filamu Tanzania, Benedict Mwegelingoha alisema ushiriki wa Bodi ya Filamu Tanzania katika onesho hilo ni sehemu ya kuendelea kuunga mkono na kuhamasisha jitihada za serikali za kukuza, kuendeleza na kuimarisha sekta ya filamu na michezo ya kuigiza nchini. 

“Bodi ya Filamu Tanzania inaendelea kuhamasisha vikundi, waandaaji, watayarishaji na waongozaji wa michezo ya jukwaani kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na matakwa ya kisheria, ikiwemo kusajili vikundi vyao na kupata vibali,” alisema Mwegelingoha. 

Ofisa huyo ambaye amemwakilisha Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, katika onesho la mchezo huo kwa kusajili vikundi vyao na kupata vibali vya maonesho kutoka Bodi ya Filamu Tanzania kutawawezesha wadau wa sekta hii kujiweka katika nafasi nzuri ya kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Filamu.

No comments