Tanzania Yaahidi Kulinda Haki za Wafanyakazi na Kuboresha Mazingira Salama ya Kazi
Tanzania imeahidi kuhakikisha inalinda haki za wafanyakazi wanaohamia nje na kuwapatia mazingira salama ya kazi.
Ahadi hiyo imetolewa Agosti 18, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, wakati akizungumza katika mkutano wa Jukwaa la Mawaziri na Kamati ya Kikanda ya Ushauri wa Kitaalamu na Sekretarieti kuhusu Uhamaji wa Nguvu Kazi.
Alisisitiza kuwa serikali imejipanga kushughulikia kikamilifu changamoto zinazowakabili wananchi wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Pia alihakikisha ushirikiano mkubwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo, baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa Jukwaa la Mawaziri wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika kuhusu Uhamaji Salama wa Nguvu Kazi.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Jinsia, Kazi na Maendeleo ya Jamii wa Uganda, Luteni Jenerali Henry Tumukunde, amesema kuwa ushirikiano wa nchi za ukanda huo utasaidia kuwa na sauti moja katika kutetea haki za wafanyakazi wanaokwenda nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM), Amy Pope, ameeleza kuwa shirika hilo lipo tayari kushirikiana na nchi za ukanda huo ili kuwajengea uwezo vijana wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi ili wawe na ujuzi unaohitajika.

Post a Comment