Siku 150 za Jaji Lila kupata majibu ya mambo matano
TUME ya Kuchunguza Wahusika na Ukiukwaji wa Sheria wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imeagizwa kuchunguza mambo matano. Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Shaban Lila amesema wamepewa siku 150 wakamilishe kazi hiyo.
Jaji Lila aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana wanatakiwa kuzitumia siku hizo kukusanya na kuchambua taarifa, kuwaita na kuwahoji watu watakaohusishwa na matukio hayo na kuandaa ripoti ambayo itawasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Tume hiyo iliundwa na Rais Samia, Mei mwaka huu kutokana na mapendekezo ya Tume ya Jaji Othman Chande iliyochunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Rais Samia aliunda Tume ya Jaji Chande kwa mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi Sura ya 32, ambapo tume hiyo iligundua mambo kadhaa ikiwamo idadi ya vifo katika vurugu zile.
Jaji Lila alisema tume hiyo imepewa hadidu za rejea tano ikiwamo ya kuchunguza na kubaini wahusika wa ghasia na namna kila mmoja alivyoshiriki katika kupanga, kufadhili, kuratibu au kutekeleza ghasia wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
“Tume itafuatilia taarifa kuhusu madai kwamba ghasia hizo zilipangwa, kuratibiwa, kufadhiliwa na kutekelezwa kwa mpango maalumu,” alieleza Jaji Lila. Aliongeza kuwa pia tume hiyo itachunguza matukio mahususi vikiwamo vifo visivyo vya kawaida vya watoto na watu wa makundi maalumu vilivyotokea katika kipindi cha uchaguzi.
Alisema pia watachunguza watu waliokuwa nje ya maeneo ya ghasia waliodaiwa kuratibu matukio hayo pamoja na watu waliopotea katika uchaguzi huo. Kwa mujibu wa Jaji Lila, tume hiyo itachunguza madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi bila kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa wakati na baada ya uchaguzi.
“Na jambo la mwisho ni kuchunguza suala lolote ambalo tume itaona ni muhimu na linalohusiana na majukumu iliyopewa,” alifafanua. “Tunautaarifu umma kwamba tume hii imeanza kazi rasmi, tunaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi… mwenye chochote, popote alipo tutamhakikishia ataifikia tume kuleta taarifa,” alibainisha.
Alisema tume ina jukumu kuu la kuchunguza na kubaini wahusika wa ghasia na ukiukwaji wa sheria uliojitokeza wakati na baada ya uchaguzi huo, pamoja na kuchunguza madhara yaliyotokana na matukio hayo ambayo ni vifo, majeruhi na watu waliopotea wakati na baada ya uchaguzi.
Alisema tume itatumia njia mbalimbali katika kukusanya taarifa ikiwamo kupokea ushahidi wa moja kwa moja kutoka kwa mtu yeyote atakayefika mbele yake, pamoja na kukagua nyaraka zitakazoonekana kuwa na uhusiano na matukio yanayochunguzwa.
Alisema ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa utafanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazohusika na kwa wale watakaotuhumiwa kwenye maelezo mbalimbali, tume itawapa nafasi kueleza kwa upande wao. “Watuhumiwa au watakaohusishwa na maelezo ya watu mbalimbali watakaojitokeza mbele ya tume nitawapa taarifa ya kuwaita,” alisema.
Jaji Lila anasaidiwa na makamishna sita ambao ni Naibu Jaji Mkuu, Jaji Rais wa Mahakama Kuu na Mjumbe wa Mahakama ya Upeo Namibia, Jaji Petrus Damaseb, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda, Jaji Barishaki Cheborion ambaye pia ni Jaji wa Rufani wa Mahakama ya Haki Afrika Mashariki iliyopo jijini Arusha. Wengine ni Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu Tanzania, Gard Mjemmas, Jaji mstaafu Awadh Bawazir, Jaji mstaafu Aishiel Sumari na Katibu wa tume hiyo ni Jaji Paul Kadushi.

Post a Comment