Latricia Ian Aondoka Kwenda Vietnam Kuwania Taji la Miss World 2026




Latricia Ian, mshindi wa kwanza wa taji la Miss World Tanzania 2026 chini ya Kampuni ya 361 Degrees Africa Limited inayomilikiwa na mwanamitindo Mustafa Hassanali, ameondoka nchini kuelekea nchini Vietnam kushiriki katika mashindano ya 75 ya kimataifa ya Miss World yatakayofanyika kuanzia Agosti 9 hadi Septemba 5, mwaka huu. 

Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 24 ameondoka akiwa na matumaini makubwa ya kurejea na taji hilo baada ya kuagwa rasmi jana, huku akibeba matumaini ya Watanzania na kusindikizwa na heri na baraka kutoka kwa wadau mbalimbali wa urembo nchini. 

Latricia anakuwa mwakilishi wa 30 tangu nchi ianze kushiriki katika ngazi ya kimataifa.

Akizungumzia safari hiyo, Mkurugenzi wa Taifa wa Miss World Tanzania, Mustafa Hassanali, alisema kuwa mrembo huyo amejitayarisha kwa bidii kubwa na kwamba atakuwa balozi mahiri wa kuitangaza Tanzania duniani kote, huku akitoa wito kwa Watanzania kuungana kwa umoja kumuunga mkono katika safari yake hiyo. 

Naye Latricia alieleza kuwa ni heshima kubwa kwake kuwakilisha taifa na kwamba amebeba bendera ya Tanzania pamoja na ndoto za wananchi wote, akiongeza kuwa amejitolea kuonyesha utamaduni, utajiri, na mabadiliko chanya ya urembo wa Kitanzania huku akitoa shukrani kwa waandaji, wadhamini, na Watanzania wote kwa ushirikiano mkubwa wanaompa. 

Kupitia ushiriki wake, uongozi wa Miss World Tanzania unathamini pia mchango wa washirika wa mpango wa Beauty With a Purpose wanaounga mkono mradi wa Nuru ya Elimu unaolenga kuwawezesha vijana kupata elimu nje ya darasa na kuleta tija katika jamii.

No comments