JAB YAZUNGUMZA NA MAAFISA HABARI WA VILABU VYA MPIRA WA MIGUU NCHINI



Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewataka Maafisa Habari wa vilabu vya mpira wa miguu nchini kuzingatia sheria, miongozo na viwango vya taaluma ya habari katika kutekeleza majukumu yao.

Akitoa mada leo Agosti 7, 2026 kuhusu majukumu ya Bodi na maadili kwa Maafisa Habari wa vilabu vya mpira wa miguu nchini, mwakilishi wa Bodi hiyo, Prudence Constantine, amesema ithibati ni nyenzo muhimu katika kutambua na kulinda maslahi ya Waandishi wa Habari, sambamba na kuimarisha weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Prudence amewataka Maafisa Habari wa vilabu wenye sifa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari kujisajili kupitia mfumo wa TAI-HABARI na kupata ithibati ili kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Sheria.

Aidha, amewashauri Maafisa Habari ambao bado hawajakidhi vigezo vinavyotakiwa kuchukua hatua za kutimiza vigezo hivyo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Sheria na viwango vya taaluma ya habari.

No comments