DC MPOGOLO AAHIDI SULUHISHO LA KUDUMU KIVUKO CHA BUCHOSA




Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amesema Kivuko cha Buchosa kilichopo Kata ya Kiwalani kitapatiwa suluhisho la kudumu, baada ya kubaini kivuko hicho kimekuwa kero kubwa kwa wananchi .

Mhe. Mpogolo ametoa ahadi hiyo wakati akikagua ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege katika Kata ya Kiwalani unaotekelezwa kupitia Mradi wa Dar es Salaam Metropolitan Development Project Phase II (DMDP II). 

Katika ziara hiyo, pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara, alitembelea eneo la Kivuko cha Buchosa na kusikiliza kilio cha wananchi kuhusu changamoto wanazokutana nazo, hususan wakati wa mvua na uhitaji wao mkubwa wa kuwa na kivuko salama na imara.

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya Wilaya ya Ilala, ambapo kupitia DMDP II imetenga zaidi ya shilingi bilioni 138 kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa takribani kilometa 48, pamoja na vivuko na madaraja. 

Amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuboresha maisha ya wananchi na kwamba changamoto nyingine zinazoibuliwa zitaendelea kushughulikiwa.

Akizungumza baada ya kuona hali halisi ya eneo hilo, Mhe. Mpogolo amesema pamoja na kuwepo kwa mahitaji ya vivuko katika maeneo mbalimbali, ni lazima hatua zianze katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

“Ni lazima tuanze mahali. Mmesema kuna vivuko vingi, lakini ukienda kwenye vivuko vyote kwa wakati mmoja unaweza usimalize kabisa. Eneo tunaloanza nalo ni kivuko hiki hapa. Nimekuja kama Mkuu wa Wilaya kuona namna gani tunatoka hapa na kupata suluhisho la kuwasaidia wananchi,” amesema Mhe. Mpogolo.

Mhe. Mpogolo amemuagiza Mhandisi John Magori Chacha, Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilala, pamoja na wataalamu wake kufika eneo la Buchosa na kufanya tathmini ya kitaalamu ili kubaini suluhisho linalofaa, huku akisisitiza kuwa ujenzi unatakiwa kuzingatia ubora, usalama na thamani ya fedha za Serikali.

 Amesema eneo la ujenzi linapaswa kupangwa vizuri ili kivuko au daraja litakalojengwa liweze kuhimili athari za maji na mvua kubwa.


No comments