DKT. MWIGULU AONGOZA HARAMBEE YA MAOMBI YA KITAIFA, ACHANGISHA MILIONI 700.
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa wito kwa Watanzania, taasisi za umma, sekta binafsi, na viongozi wa dini kuwekeza katika malezi, uadilifu, na uwajibikaji kama mhimili mkuu wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Agosti 29, 2026) wakati wa hafla ya uchangiaji wa maandalizi ya Ibada ya Kitaifa ya Chakula cha Asubuhi na Maombi (Tanzania National Prayer Breakfast), iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam, akifanikisha kuchangishwa kwa shilingi milioni 700.
Akizungumza katika harambee hiyo, Dkt. Mwigulu amesema kuwa maombi hayo yanayoratibiwa na Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT) yamekuwa na tija kwa Taifa katika kujenga maadili, uzalendo, na uwajibikaji miongoni mwa Watanzania.
"Ingawa utekelezaji wa miradi ya miundombinu, kilimo, afya, elimu, na teknolojia ni muhimu, lakini maendeleo ya kweli katika Taifa yanategemea amani, haki, utulivu, na uongozi bora wenye uwezo wa kusimamia rasilimali za umma kwa uwazi."
"Hatuwezi kuendelea iwapo muda mwingi tunatumia kuvutana, kushindana, kutofautiana au kuwekeza katika kuandaa jamii iliyo njema na hili si jambo tu la Serikali wala si jambo la viongozi wetu wa dini peke yao, hili ni jambo la kila familia, ni jambo la kila mtu. Kwa hiyo, hata tuliokusanyika leo hapa tunachangia kwa namna moja katika maandalizi haya. Maana yake, tunapotaka kujenga taifa linalotanguliza utu, haki, uwajibikaji, amani, na mshkamano, ni lazima tuanzie kwenye kuwaandaa Watanzania," amefafanua Waziri Mkuu.
Akihusianisha tukio hilo linalotarajiwa kuwakutanisha zaidi ya watu 3,000 na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, Dkt. Mwigulu ameeleza kuwa yanahitaji mabadiliko ya kifikra na mtindo wa ufanyaji kazi usio wa mazoea.
"Jambo hili limekuja katika muda mwafaka, ambapo ndiyo kwanza tunaanza utekelezaji wa dira mpya, Dira ya 2050. Na kama mnavyojua, dira hii ina malengo makubwa, kwa Kiingereza wanasema we are big ambitious, but yet it is achievable. Hiyo inatuhadharisha tu kwamba tumeweka malengo makubwa, tunatakiwa tufanye kazi kwa namna isiyo ya kawaida, isiyo ya mazoea," amehimiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali zilizoyakumba mataifa mbalimbali duniani, bado Tanzania imeendelea kuwa na ustahimilivu wa uchumi wa Taifa.
"Nchi yetu imeonesha ustahimilivu kutokana na uwepo wa uongozi bora, sera pamoja na kujituma kwa Watanzania katika ujenzi wa taifa. Kwa hiyo, nitoe wito kwa wadau wote kuunga mkono ajenda ambazo zimeletwa na ndugu zetu hapa kwa sababu tunasisitiza misingi iliyo bora ambayo itaendelea kusukuma taifa letu mbele," ameeleza Dkt. Mwigulu.
Akigusia maandalizi ya maombi hayo ya Novemba 2026, Dkt. Nchemba amezialika taasisi na wadau kujitokeza kuchangia kufanikisha ajenda hiyo ili kuijenga Tanzania bora ya leo na kesho.
Kwa upande wake mlezi wa KLNT, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye amesema Tanzania National Prayer Breakfast ni programu inayolenga kufanya uwekezaji wa taifa kwa kizazi kijacho, ili Tanzania ya kesho iwe salama, yenye upendo, mshikamano, na yenye maendeleo makubwa zaidi.
"Mheshimiwa Mgeni Rasmi, taifa lolote haliwezi kusimama juu ya sera nzuri, mipango mizuri, au hata bajeti nzuri peke yake. Pamoja na hayo, muhimu zaidi ni uwepo wa hofu ya Mungu, viongozi waliojengwa na kuandaliwa na wazalendo wa kweli kwa taifa lao. Kwa hiyo, tunapokutana hapa leo, tunayapandikiza hayo kwa Tanzania ya kesho," amesema Sumaye.

Post a Comment