DK NCHIMBI ASISITIZA UKWELI WENYE NIA NJEMA YA KUJENGA NCHI MAZIKO YA MAKENE



 Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amewataka Watanzania kuwa huru kutoa mawazo yao kwa nia njema bila kuficha ukweli, akisema utamaduni wa kusema ukweli na kutoa ushauri wa kujenga utaisaidia nchi kupata maendeleo makubwa zaidi. 

Dk Nchimbi alisema hayo wakati akitoa salamu za rambirambi katika mazishi ya Boniface Makene, aliyewahi kuwa mwandishi wa habari wa Makamu wa Rais mstaafu, Mohamed Gharib Bilal yaliyofanyika katika Kijiji cha Mabui Merafuru wilayani Musoma mkoani Mara.

Akizungumza katika ibada ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Agustino Mabui Merafuru, Dk Nchimbi alisema Makene alikuwa mtu aliyependa kusema ukweli na kutoa ushauri wenye lengo la kujenga bila kujali namna utakavyopokelewa.






Dk Nchimbi alisisitiza kuwa ni muhimu kuwa na Watanzania wengi wenye ujasiri wa kutoa mawazo yao kwa nia njema bila kuficha ukweli kwa sababu utaratibu huo utasaidia kuijenga nchi kwa kiwango kikubwa, huku akiongeza kuwa kila mwananchi anapaswa kuona ana nafasi ya kushiriki katika ujenzi wa taifa kwa kutoa mawazo, ushauri na maoni yatakayosaidia maendeleo. 

Aidha, alitoa pole kwa familia ya marehemu pamoja na waombolezaji wote walioguswa na msiba huo, akieleza kuwa taifa limepoteza mtu mwenye mchango mkubwa katika sekta ya habari na ushauri wa uongozi.

Makamu wa Rais pia aliwashukuru Watanzania waishio nje ya nchi kwa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha mwili wa marehemu Makene unarejeshwa nchini kwa ajili ya mazishi, na aliwataka kuendelea kushirikiana, kupendana na kukumbuka kuwa Tanzania ndiyo taifa lao wakati wote. Awali, akitoa mahubiri wakati wa ibada ya mazishi, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Agustino Mabui Merafuru, Padri Peter Maraga alisema Makene atakumbukwa kwa kutumia vipawa vyake kuwahudumia watu wengine na kuwataka waumini kuendelea kutumia vipaji walivyopewa katika kuwatumikia wenzao na jamii kwa ujumla.


No comments