DANGOTE AIPONGEZA SERIKALI, AANGAZIA FURSA ZAIDI ZA UWEKEZAJI NCHINI
Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaji Aliko Dangote, ameipongeza kwa dhati Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, pamoja na utatuzi wa haraka wa changamoto zinazowakabili wawekezaji nchini.
Alibainisha kuwa hatua zilizochukuliwa na Serikali kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili shughuli za Kiwanda cha Saruji cha Dangote mkoani Mtwara zimeongeza tija, ufanisi wa uendeshaji, na kuimarisha imani ya kampuni hiyo kwa Tanzania kama eneo salama na la kimkakati la uwekezaji barani Afrika.
Alhaji Dangote alimshukuru Rais Samia akisema kuwa wakati anaingia madarakani kulikuwa na changamoto nyingi, lakini kama alivyokuwa ameahidi, kila changamoto imeshughulikiwa ipasavyo.
Alhaj Dangote alisema hayo katika mazungumzo yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, , Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kuhusu utendaji wa kiwanda hicho cha saruji, Alhaji Dangote ameeleza kuwa kinaendelea kufanya vizuri na kinatarajia kuzalisha takribani tani milioni 2.8 kwa mwaka huu, kikitishia kufikia lengo lake kuu la kuzalisha tani milioni 3.2.
Katika kuunga mkono matumizi ya nishati safi na mbadala, Dangote Group tayari imeleta nchini malori 400 yanayotumia gesi asilia kwa ajili ya kusafirisha na kusambaza saruji, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kubadilisha jumla ya malori 700 ya kampuni hiyo kwenda kwenye matumizi ya gesi ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Dangote aliongeza kuwa bila uongozi thabiti wa Rais Samia, soko lisingekuwa bora na lenye tija ya kuiwezesha kampuni hiyo kufanya biashara kwa ukubwa huo.
Mbali na uwekezaji uliopo, mazungumzo hayo yameangazia fursa mpya ambapo pande zote mbili zimejadili uwezekano wa Dangote Group kuingia ubia na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza mradi mkubwa wa kusafisha mafuta ghafi unaokadiriwa kugharimu takribani Dola za Marekani bilioni 17.
Mradi huo mkubwa unatarajiwa kunufaisha nchi za Afrika Mashariki na Ethiopia, huku ukitoa fursa kwa nchi hizo za ukanda kushiriki kupitia umiliki wa hisa kama sehemu ya kujenga uwezo wa bara la Afrika kujitosheleza kwa uzalishaji wa mafuta, kupunguza utegemezi kutoka nje, na kujilinda dhidi ya athari za misukosuko ya bei na upatikanaji wa bidhaa hizo.
Kwa upande wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemhakikishia Alhaji Dangote ushirikiano wa kutosha kutoka serikalini na kumuomba kuendelea kuangalia fursa zaidi za biashara na uwekezaji nchini zenye tija na manufaa kwa mwekezaji, Serikali, na Taifa kwa ujumla.
Halikadhalika, Rais Samia ameikaribisha rasmi Dangote Group kuwekeza katika sekta ya uzalishaji wa mbolea nchini, akibainisha kuwa kwa sasa mahitaji ya bidhaa hiyo hapa nchini ni makubwa mno kuliko uwezo wa sasa wa uzalishaji wa ndani.
Post a Comment