Buganga ateta na mwanamuziki Fobby fursa Afcon
Mwangaza wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizopangwa kufanyika nchini mwaka 2027 umeanza kuamsha ari kubwa ya ubunifu, huku mamlaka za sanaa zikihamasisha matumizi ya fursa hiyo adhimu.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Edward Buganga, ametoa mwito kwa wasanii na wadau wote wa tasnia ya ubunifu nchini kujifunga mkanda na kuzalisha kazi zenye viwango vya juu ambazo hazitakuwa tu burudani, bali zitaleta tija kubwa katika kuitangaza nchi yetu kimataifa wakati wa mashindano hayo makubwa ya soka.
Buganga amebainisha kuwa sanaa ina nguvu ya kipekee ya kubeba taswira ya taifa, na kipindi hiki ni muafaka wa kuonyesha ulimwengu utajiri wetu wa kitamaduni.
Sauti hii ya kiongozi wa baraza imerejelewa wakati wa kikao maalum kilichofanyika katika ofisi za BASATA, ambapo alikutana na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Frank Ngumbuchi maarufu kama ‘Fobby’.
Msanii huyo kijana alifika makao makuu ya baraza hilo kuwasilisha rasmi kazi maalum ya muziki aliyoiandaa kwa ajili ya mashindano hayo ya AFCON 2027, akiwa na lengo la kutumia vipaji vyake kama zana ya uzalendo ya kuitangaza Tanzania duniani.
Mazungumzo yao yalijikita katika kuchambua fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii zilizopo kupitia sanaa ya muziki, ambayo inatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha burudani kwa maelfu ya wageni watakaomiminika nchini.
Katika mazungumzo hayo, Buganga alimwagia sifa kedekede msanii huyo kwa kuonyesha mfano bora wa ukomavu kwa kujirasimisha kisheria na kuhuisha kibali chake cha kufanya kazi za sanaa, jambo ambalo ni msingi wa kulinda haki na maslahi ya kazi zake.
Kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kumhimiza Fobby kutobaki peke yake bali kuwa nguzo na daraja la kuinua vijana wengine wenye vipaji mtaani kupitia jukwaa lake la sanaa. Alisisitiza kuwa ujio wa mashindano haya ya bara la Afrika utafungua milango ya kiuchumi kupitia sekta mbalimbali za ubunifu, hivyo ni lazima wasanii wote nchini wachangamkie fursa hii ili kukuza vipato vyao na kuongeza mchango wa sanaa katika pato la taifa.
Huku maandalizi yakishika kasi, Buganga alifafanua kuwa ujio wa wageni utakuwa na maana kubwa ikiwa wataondoka na kumbukumbu nzuri ya ukarimu na uzuri wa nchi yetu kupitia kazi za sanaa watakazokutana nazo.
Alitoa rai kwamba, wakati wasanii wakitengeneza kazi zitakazoleta tija na kuvutia wageni, hawapaswi kusahau kulinda na kudumisha maadili na misingi ya utamaduni wa Kitanzania. Hali hii itaifanya nchi yetu kuwa kivutio cha kipekee kinachochanganya msisimko wa michezo na ustaarabu wa kiutamaduni.
Kwa upande wake, msanii Fobby alitoa shukrani za dhati kwa serikali kwa namna inavyojali na kusimama mstari wa mbele kuhakikisha sanaa ya Tanzania inasonga mbele na kuwa chanzo rasmi cha ajira kwa maelfu ya vijana nchini. Alieleza kuwa siri ya mafanikio na usalama wa msanii ni kufuata taratibu zilizowekwa, na ndio maana yeye binafsi amehakikisha amesajiliwa na kuwa na vibali vyote vinavyotakiwa. Alitoa wito kwa wasanii wenzake kote nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea, wajirasimishe haraka, na kutambua kuwa wao ni vioo vya jamii ambao wanabeba jukumu zito la kuonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kutumia sanaa zao kama silaha kuu ya kuitangaza Tanzania wakati wa AFCON 2027.

Post a Comment