TANZANIA NA GHANA KUIMARISHA USHIRIKIANO KIUCHUMI NA AJIRA KWA VIJANA
TANZANIA na Ghana zimekiubaliana kuongeza ushirikiano katika maendeleo ya ujuzi, ubunifu, na ujasiriamali.
Pia zimezungumzia umuhimu wa kuongeza thamani ya rasilimali za ndani badala ya kuendelea kuuza malighafi nje ya nchi.
Hayo yamejiri wakati wa mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mheshimiwa John Dramani Mahama, Arusha leo.
Taarifa kutoka Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari imesema katika mazungumzo ya pande mbili yaliyofanyika Ikulu ya Arusha tarehe 02 Machi, 2026, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuweka mazingira bora ya uwekezaji yatakayozalisha ajira endelevu kwa vijana wa pande zote mbili.
Aidha taarifa hiyo ya Ikulu imesema mazungumzo hayo yamejikita katika kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, hususan katika mageuzi ya kiuchumi, ajira kwa vijana, na maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
Katika mazungumzo hayo Rais Mahama ameelezea hatua zinazochukuliwa na Ghana katika kuimarisha usimamizi wa sekta za madini na kakao kwa lengo la kuongeza mapato ya ndani na kukuza uchakataji wa ndani. Kwa upande wake, Rais Samia amesema Tanzania inaendelea kuharakisha mkakati wa uchumi wa viwanda, ikiwemo kuongeza thamani ya mazao ya kimkakati kama pamba na kuimarisha uchakataji wa madini.
Rais Samia amebainisha kuwa Tanzania ina nafasi muhimu ya kujifunza kutoka Ghana katika usimamizi wa rasilimali na sera za uchumi wa ndani.
Kuhusu eneo la uchumi, Rais Samia amesisitiza dhamira ya Tanzania ya kuimarisha mifumo ya fedha za kidijitali na usalama wa mitandao kama sehemu ya mkakati wa kujenga uchumi shindani na jumuishi. Amesema serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA na kukuza ubunifu wa vijana, akibainisha kuwa uzoefu wa Ghana katika sekta ya teknolojia ya fedha na ulinzi wa miundombinu ya kimtandao ni eneo muhimu la kujifunza na kushirikiana ili kuongeza ujumuishaji wa kifedha nchini.
Vilevile, viongozi hao wamepongeza hatua ya kuimarisha usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) kati ya Tanzania na Ghana. Wamesema kuwa hatua hiyo itarahisisha biashara, utalii, na mwingiliano wa watu kati ya nchi hizo mbili, huku wakisisitiza kuwa safari hizo za moja kwa moja zitachochea biashara si tu kwa nchi hizo, bali pia ndani ya Bara la Afrika.
Rais wa Ghana yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja, ambapo anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama na Maadhimisho ya Miaka 20 ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu yenye makao makuu yake jijini Arusha.
Post a Comment