Vurugu za Fainali ya AFCON 2025, mahakama yawatupa jela mashabiki 19
Mahakama nchini Morocco imewahukumu vifungo vya hadi mwaka mmoja gerezani mashabiki 19 wa soka kufuatia matukio ya kihuni yaliyovuruga fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kati ya wenyeji Morocco na Senegal.
Washitakiwa hao, ambao ni raia 18 wa Senegal na raia mmoja wa Ufaransa, walipatikana na hatia ya makosa kadhaa baada ya kikao cha mahakama kilichodumu kwa zaidi ya saa tano siku ya Alhamisi.
Mashabiki hao walikamatwa mara baada ya fainali hiyo iliyopigwa Januari 18 na wamekuwa mahabusu kwa zaidi ya mwezi mmoja wakikabiliwa na tuhuma za kuharibu miundombinu ya michezo na kufanya fujo uwanjani.
Katika kutoa hukumu hiyo, wakili Naima El Guellaf ameeleza kuwa washitakiwa 11 wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani na faini ya dola 550 kila mmoja. Wengine wanne wamepewa kifungo cha miezi sita na faini ya dola 218, huku wanne waliobaki wakihukumiwa miezi mitatu jela na faini ya dola 130.
Ripoti zinaeleza kuwa kulizuka hali ya simanzi mahakamani hapo baada ya hukumu kusomwa na mshitakiwa mmoja alizimia baada ya kusomewa hukumu hiyo huku ndugu wa washitakiwa wakisisitiza kuwa wapendwa wao hawana hatia.
Upande wa mashtaka uliomba adhabu kali zaidi ukihoji kuwa mashabiki hao walisababisha usumbufu mkubwa uwanjani na uharibifu wa mali wenye thamani inayozidi dola 476,719.
Kwa upande mwingine, mawakili wa utetezi walidai kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani wateja wao. Wanadiplomasia kutoka Senegal na Ufaransa walihudhuria kikao hicho, na mawakili tayari wamethibitisha kuwa watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.
Vurugu hizo zilizozua taharuki zilianza baada ya Morocco kuzawadiwa mkwaju wa penalti katika dakika za nyongeza mwishoni mwa mchezo, jambo lililopelekea wachezaji wa Senegal kugoma na kutoka nje ya uwanja kulalamikia uamuzi huo.
Mashabiki wenye hasira walianza kurusha viti uwanjani na kupambana na walinzi kabla ya jeshi la polisi kuingilia kati kuzuia umati uliokuwa unajaribu kuvamia dimba la Rabat.
Licha ya vurugu hizo, kipa wa Senegal, Edouard Mendy, aliokoa penalti hiyo iliyopigwa na Brahim Diaz, na kufuatiwa na bao la Pape Gueye katika muda wa nyongeza lililoipa Senegal ushindi wa 1-0.
Hata hivyo, matukio hayo ya aibu yameifanya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kupiga faini ya dola milioni moja kwa mashirikisho ya soka ya Senegal na Morocco, huku Morocco ikitangaza kupinga adhabu hiyo ikidai kuwa ni kubwa mno kulingana na tukio lenyewe.

Post a Comment