VIONGOZI VYAMA VYA WAFANYAKAZI ZINGATIENI SHERIA NA KATIBA ZENU: SANGU




Na: OWM (KAM) – Dodoma

Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi, Waajiri na Shirikisho nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuzingatia sheria na katiba za vyama vyao ili kuendelea kuleta ustawi na tija sehemu za kazi pamoja na kukuza ushirikiano na serikali.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu amewataka viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na katiba za vyama vyao. 

 Waziri Sangu amesema hayo leo Februari 17, 2026 katika kikao kazi cha Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, Waajiri na Shirikisho kilichofanyika jengo la PSSSF, jijini Dodoma ambapo alisisitiza kuwa uongozi bora na uwajibikaji unajengwa kwa kuheshimu misingi ya kisheria na taratibu zilizowekwa, hivyo husaidia kuimarisha mahusiano ya kazi na kulinda maslahi ya wafanyakazi pamoja na waajiri.

Vilevile, Waziri Sangu amehamasisha viongozi hao kutekekeza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ili kujenga uchumi shindani, jumuishi na kukuza teknolojia. Amesema ili kufikia malengo hayo, ni lazima maeneo ya kazi na soko letu la ajira liwe na utulivu na tija ya hali ya juu ili kuendelea kuongeza ubora wa utoaji huduma na uzalishaji bidhaa zenye ushindani.

Kwa upande mwengine, Waziri Sangu amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya ustawi wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri ili kuwa na faida ambayo itajenga maslahi bora, usalama wa kijamii na mazingira bora ya kazi.

Akizungumza awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mary Maganga amesema kikao kazi hicho kililenga kuimarisha dhana ya Utatu, ambayo ndiyo nguzo kuu ya amani ya sehemu za kazi na ustawi wa soko la ajira nchini.



Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amesema kuwa shirikisho hilo linaendelea kusimamia maslahi ya wafanyakazi nchini na kukuza tija mahali pa kazi ambapo wataendelea kushirikiana na Serikali na waajili kutatua changamoto zilizopo kwa njia ya mazungumzo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utafiti, Sera na Mipango (ATE), Renatus Mbamilo akizungumza kwa niaba ya Chama cha Waajiri Tanzania alisema chama hicho  kinaendelea kutekeleza majukumu  yake kwa kuzingatia Sheria na Mpango Mkakati wa ATE ambao umejengwa kwa kuakisi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mpango wa Kitaifa wa Kazi zenye Staha na kwamba wataendelea kutoa elimu kwa waajiri juu ya taratibu za kazi.

Mwakilishi wa Vyama vilivyo Nje ya TUCTA, Michael Pamagi ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwezesha kufanyika kwa kikao kazi hicho ambacho kitasaidia kujenga mfumo imara wa mahusiano kazini unaozingatia haki na wajibu kwa wadau wa utatu.

Kikao kazi hicho cha siku moja kiliitishwa na Waziri Sangu kwa ajili ya kuzungumzia masuala muhimu kwa vyama hivyo na Kuendeleza dhamiria ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kujenga mahusiano chanya baina ya serikali na wadau wa utatu ili kufikia malengo ya kukuza ari ya kazi na utu miongoni mwa wafanyakazi nchini ambapo jumla ya viongozi 150 walishiriki.


No comments