‘VIJANA PLATFORM’ SINGIDA YAZINDULIWA: VIJANA WATAKIWA KUTHUBUTU





WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amewataka vijana nchini kuacha tabia ya kukata tamaa na badala yake waonyeshe uthubutu wa hali ya juu kwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Akizungumza  Februari 12, 2026, wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Vijana kwa wanafunzi wa Vyuo na Vyuo Vikuu (Vijana Platform Campus Connect) mkoani Singida, Waziri Nanauka amesisitiza kuwa fursa za maendeleo nchini si kwa ajili ya kundi maalum la watu, bali ni kwa kila kijana mwenye nia na uthubutu.

"Nawaasa vijana wenzangu, acheni kuamini kuwa fursa fulani ni kwa ajili ya vijana maalum. Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa kila mmoja. Jukwaa hili la Vijana Platform ni nyenzo yenu ya kuanzisha miradi, kushiriki mijadala ya kimaendeleo na kupata taarifa sahihi za fursa za serikali," alisema Mhe. Nanauka.

Wito wa Waziri Nanauka unakuja wakati ambapo Serikali imefanya mageuzi makubwa ya kisheria na kiuchumi ili kuwasaidia vijana wanaochipukia katika ulimwengu wa kidijitali. 

Katika Mkutano wa Mwaka wa Utangazaji (ABC 2026) unaoendelea Dodoma, Serikali imetangaza kupunguza ada za leseni kwa watoa maudhui mtandaoni kutoka shilingi laki tano hadi elfu hamsini pekee, hatua ambayo ni mkombozi kwa vijana wabunifu.

Kwa upande wao, Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) umepokea wito huo kwa vitendo, ukiweka mkakati wa kutumia kundi lake la "Mabalozi wa Kidijitali" kuelimisha vijana kuhusu namna ya kutumia Akili Unde (AI) na majukwaa ya kijamii kujiingizia kipato halali huku wakilinda taswira ya taifa.

Waziri Nanauka  ameahidi kuwa Ofisi ya Rais itaendelea kuratibu majukwaa hayo ya Campus Connect nchi nzima ili kuhakikisha sauti na mawazo ya vijana yanakuwa sehemu ya mipango ya maendeleo kuelekea Dira ya 2050.


No comments