UTALII WA MELI WAWAHAKIKISHIA VIJANA WA KILWA UFUNGUO WA AJIRA




Mambo yanazidi kunoga katika sekta ya utalii nchini Tanzania baada ya Bandari ya Kilwa, mkoani Lindi, kuipokea meli ya kitalii ya Le Bellot ikiwa na watalii zaidi ya 150 kutoka mataifa mbalimbali duniani. 

Mapokezi haya makubwa yaliyounganisha Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyapori (TAWA), na wadau wa sekta binafsi, yanalenga kuimarisha utalii wa meli na kutangaza utajiri wa kihistoria wa Magofu ya Kilwa Kisiwani.

Hii ni meli ya pili kupokewa nchini ndani ya kipindi kifupi, baada ya meli nyingine iliyobeba watalii zaidi ya 500 kuwasili hivi karibuni, hali inayothibitisha kuwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi unachochea kasi mpya ya ukuaji wa uchumi wa bluu kote Bara na Zanzibar.

Kushamiri huku kwa utalii kumeambatana na ujumbe mzito kutoka kwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, aliyewasihi vijana kuchangamkia fursa badala ya kulalamika. 

Akizungumza Februari 12, 2026, Msigwa amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mazingira wezeshi, ikiwemo kuwapatia vijana wizara yao rasmi ili iwe chimbuko la kujikomboa kiuchumi. 

Ujumbe huu ni wito kwa vijana kuitambua nafasi yao kama nguvu kazi ya taifa na kutumia kila fursa inayojitokeza katika sekta ya utalii na maeneo mengine ili kujiinua kimaisha.

Katika kuitikia wito huo, vijana nchini, hususan wa mikoa ya pwani kama Lindi, wana nafasi ya kipekee ya kugeuza utalii huu kuwa chanzo cha mapato kupitia shughuli mbalimbali. 

Badala ya kusubiri ajira za ofisini, vijana wanaweza kujiingiza katika kutoa huduma za mwongozo wa watalii kwa kutumia maarifa ya historia yetu, au kuanzisha miradi ya usafirishaji wa kisasa baharini na nchi kavu. 

Aidha, fursa zipo katika sanaa na ufundi kwa kutengeneza bidhaa za asili, kuanzisha migahawa ya vyakula vya asili vyenye viwango vya kimataifa, na kutumia teknolojia katika upigaji picha na masoko ya kidijitali ili kuitangaza Tanzania duniani. 

Kwa kufanya hivi, vijana hawatatengeneza tu ajira, bali watakuwa injini muhimu ya kuimarisha sekta ya utalii na kuitokomeza njaa nchini.


No comments