POLISI YATOA ONYO USAMBAZAJI HABARI ZA UONGO NA TAHARUKI MITANDAONI,PICHA INAYOTEMBEA NI YA MWAKA 2023



Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa onyo kali dh
idi ya watu na vikundi vinavyojihusisha na usambazaji wa picha mjongeo (video) na taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kuzua taharuki na hofu miongoni mwa wananchi. 

Polisi imesisitiza kuwa vitendo hivyo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi na vinalenga kuvuruga amani na utulivu, huku ikiwataka wananchi kuwa mstari wa mbele kusaidia kukomesha tabia hiyo kwa kutoa taarifa sahihi na kutojihusisha na usambazaji wa maudhui wasiyokuwa na uhakika nayo.

Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Februari 22, 2026, na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, amefafanua kuwa video inayosambazwa hivi sasa ikionyesha matukio ya ukatili si ya sasa, bali ni tukio la zamani lililotokea mkoani Dodoma mwaka 2023. 

DCP Misime amebainisha kuwa tayari hatua stahiki za kisheria zilichukuliwa dhidi ya wahusika wote wa tukio hilo la mwaka 2023, hivyo kuirejesha video hiyo na kuifanya ionekane ni ya sasa ni upotoshaji wa makusudi wenye nia mbaya kwa usalama wa jamii.

Aidha, Jeshi la Polisi limetumia fursa hiyo kutolea ufafanuzi taarifa nyingine potofu zinazodai kutekwa kwa Mchungaji Yanick Mbombo Cele, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), jijini Dar es Salaam. 

Polisi imeweka wazi kuwa mchungaji huyo alikamatwa Mei 15, 2025 kwa makosa mazito ikiwemo ubakaji na udanganyifu, na baada ya kukiri makosa yake kupitia mfumo wa majadiliano (plea bargaining) na kulipa faini, alishafukuzwa nchini kisheria kupitia Idara ya Uhamiaji. Polisi wameelezea kushangazwa na madai ya kutekwa kwa mtu ambaye kimsingi hapaswi kuwepo nchini na kuwataka wanaosambaza uzushi huo kuacha mara moja.

Katika hatua ya kuimarisha usalama, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za kweli pindi wanapohisi kuna viashiria vya uhalifu badala ya kukimbilia mitandaoni kusambaza hofu. Polisi imesisitiza kuwa inaendelea kufuatilia kwa karibu mitandao yote na itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kuratibu au kusambaza taarifa zinazolenga kuaminisha jamii mambo yasiyo ya kweli.

Hatua hizi za Polisi zinaendana na msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, inayolenga kudumisha amani na utulivu kama msingi mkuu wa maendeleo ya taifa. Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa amani na usalama ni jukumu la kila mwananchi ili kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kuendelea bila hofu, huku ikihimiza matumizi sahihi ya teknolojia kwa ajili ya ustawi wa taifa.

No comments