SAFARI YA VIJANA WA NJOMBE KUTOKA KUPONDA KOKOTO HADI KIWANDA CHA CHUMA



Safari ya kimaendeleo kwa vijana wa Mkoa wa Njombe imekuwa kielelezo cha namna maisha yalivyo mchakato unaohitaji uvumilivu na uthubutu. 

Kikundi cha vijana mkoani humo kimeanza safari yake kwa kazi ngumu ya kuponda kokoto kwa kutumia nyundo za mikono, lakini kutokana na nia yao ya dhati ya kujikwamua, waliomba mkopo wa kwanza wa shilingi milioni 10 kutoka halmashauri na kufanikiwa kuupata. Baada ya kufanya vizuri, waliomba tena mkopo wa shilingi milioni 20 na sasa wamepata shilingi milioni 50, fedha ambazo zimewawezesha kununua mitambo ya kisasa ya kupondea kokoto na kuachana na upondaji wa mikono.

Mipango ya vijana hao kwa sasa ni mikubwa zaidi kwani wanajipanga kumiliki kiwanda cha kati cha chuma kitakachozalisha vifaa vya mashambani, wakiamini kuwa kesho yao ina nuru na maendeleo yao yatawafanya waipende zaidi nchi yao na kuwa walinzi wa amani. 

Wakati vijana hao wa nNjombe wamesema wanafurahi kwa jinsi mikopo ya halmashauri ilivyowanyanyua, vijana wengine wamemtaka Waziri mwenye dhamana na vijana kuwasaidia kutimiza ndoto kwani mifumo ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inawanyoosha. 

Wanadai kuwa mifumo ya sasa ya kujaza taarifa mtandaoni inawalazimu kutumia gharama kubwa kuwalipa washauri wa kodi ili kuwasaidia, jambo linalowarudisha nyuma kiuchumi badala ya fedha za mikopo kuwasaidia kujikwamua.

Vijana hao wameeleza kuwa taratibu za kodi zinapaswa kuwa rafiki kwa kampuni changa na viwanda vidogo vinavyoanza kujitafuta.

Wanapendekeza TRA iweke utaratibu wa kuwakadiria kodi kulingana na ukubwa wa biashara zao kuliko kuwalazimisha kutumia mifumo inayohitaji gharama za ziada za kitaalamu wakati bado wanapambana kulinda mitaji yao midogo. 

Ombi lao kwa serikali ni kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuwakwamua hazirudi tena serikalini kupitia gharama za uendeshaji wa mifumo ya kodi, ili waweze kufikia lengo lao la kuwa na taifa jipya lenye viwanda vinavyomilikiwa na wazawa

No comments