MWANAFA AZINDUA LIGI YA RAMADHANI DAR, AAHIDI MAPINDUZI YA MIUNDOMBINU
SERIKALI imesisitiza dhamira yake ya dhati ya kuigeuza sekta ya michezo, hususan mpira wa kikapu (Basketball), kuwa chanzo kikubwa cha uchumi na ajira kwa vijana nchini kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), wakati akizindua rasmi msimu wa mwaka 2026 wa Ligi ya Nyota wa Kikapu ya Ramadhani. Uzinduzi huo uliofanyika juzi katika viwanja vya Don Bosco, jijini Dar es Salaam, uliambatana na shamrashamra kutoka kwa wanamichezo na mashabiki wa mchezo huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, MwanaFA aliweka wazi kuwa Serikali inatambua kasi ya kukua kwa umaarufu wa mchezo wa kikapu nchini, hivyo imejipanga kuweka mazingira wezeshi yatakayosaidia kuibua na kukuza vipaji vipya kuanzia ngazi ya chini.
Mpango Mkakati wa Miundombinu
MwanaFA alieleza kuwa serikali ina mpango thabiti wa kujenga na kuboresha viwanja vya kikapu ili viweze kukidhi viwango vinavyohitajika kutoa sapoti kwa wachezaji. Alisisitiza kuwa maboresho hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha vijana wanapata sehemu bora za kufanyia mazoezi na mashindano.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa michezo katika taifa letu. Tuna mpango thabiti wa kujenga na kuboresha miundombinu itakayosaidia mchezo huu wa mpira wa kikapu,” alisema Naibu Waziri huyo.
Michezo kama Chanzo cha Ajira
Aidha, Mhe. Mwinjuma alifafanua kuwa uwekezaji huo haulengi tu burudani, bali ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha sekta ya michezo inachangia kikamilifu kwenye pato la taifa na kutoa ajira za uhakika. Alisema lengo kuu ni kuona vijana wa Kitanzania wanatumia vipaji vyao kujikwamua kiuchumi na kuendesha maisha yao kupitia mpira wa kikapu.
“Lengo letu siyo tu kukuza vipaji, bali ni kuhakikisha michezo inakuwa sehemu ya uchumi na inatoa fursa za ajira za uhakika kwa vijana wetu,” aliongeza MwanaFA, huku akitoa wito kwa wadau wa michezo kuendelea kushirikiana na serikali katika kukuza mchezo huo.
Uzinduzi wa Ligi ya Nyota wa Kikapu ya Ramadhani unatajwa kuwa ni jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano miongoni mwa vijana na kutoa burudani safi wakati wa msimu huu, huku ukiongeza hamasa ya mchezo huo nchini.

Post a Comment