KAREMA KUANZA KUNG’ARA: MELI MPYA KUCHANGAMSHA BIASHARA YA DR CONGO, BURUNDI NA ZAMBIA




Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amemwaga pongezi kwa hatua kubwa ya ujenzi wa meli nne mpya katika Bandari ya Karema, wilayani Tanganyika, mkoani Katavi. 

Mradi huo, ambao ni matunda ya ubia kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kampuni ya Gold Voyage Logistics ya nchini China, unalenga kubadilisha uso wa usafirishaji katika Ziwa Tanganyika.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo , Mhe. Kihenzile amebainisha kuwa meli hizo ni mkombozi wa kiuchumi kwani zitakuwa kiunganishi muhimu cha mizigo kutoka nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, na Zambia. Alisisitiza kuwa mzigo huo utapitia bandari za Ziwa Tanganyika kuelekea Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirishwa kwenda masoko ya kimataifa, jambo litakaloongeza tija na mapato kwa taifa.

Aidha, Naibu Waziri huyo ametoa mwito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya uchukuzi. Alieleza kuwa ushiriki wa wadau binafsi ni nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi wa usafiri na usafirishaji, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara na miundombinu imara ili kuvutia mitaji zaidi.

Awali, Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula, aliwasilisha taarifa ya ujenzi huo akibainisha kuwa meli tatu tayari zimekamilika kwa asilimia mia moja. Aidha, meli ya nne imefikia asilimia 90 ya ujenzi wake na inatarajiwa kuanza kazi muda mfupi ujao, hatua itakayokamilisha kikosi hicho cha meli nne kilichokusudiwa kuimarisha usafirishaji ziwani humo.

Licha ya ujenzi kuendelea, Mabula alieleza kuwa Bandari ya Karema tayari imeanza kuonesha cheche baada ya kuhudumia tani 15,000 za mizigo, meli saba, na takribani boti 600 tangu kuanza kwake. Alibainisha kuwa takwimu hizo ni mwanzo tu, kwani kukamilika kwa miundombinu yote kutaifanya bandari hiyo kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu na kutoa huduma ambazo hazijawahi kushuhudiwa hapo awali.

No comments