Makonda: Asilimia 40 ya Wanafunzi Duniani Hawasomi kwa Lugha Wanayoielewa



Takwimu zinaonyesha kuwa takribani asilimia 40 ya wanafunzi duniani kote hawapati elimu kupitia lugha wanayoielewa vizuri, jambo ambalo ni changamoto kubwa inayohitaji hatua za makusudi ili kuimarisha uwezo wa watoto kufikiri na kujiamini kupitia lugha-mama. 

Akibainisha changamoto hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Paul Christian Makonda, amesisitiza kuwa matumizi ya wingilugha ni nguzo muhimu ya amani na mshikamano wa jamii. 

Mheshimiwa Makonda ametoa kauli hiyo leo tarehe 20 Februari 2026 jijini Paris, Ufaransa, alipohutubia Maadhimisho ya 26 ya Siku ya Kimataifa ya Lugha-Mama kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika hotuba yake iliyowasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa UNESCO, Waziri Makonda alieleza kuwa lugha-mama si tukio la kumbukumbu pekee bali ni chachu ya mabadiliko kuelekea usawa na maendeleo. 

Alifafanua kuwa lugha ya Kiswahili, ambayo sasa inazungumzwa na watu zaidi ya milioni 500 duniani, inaendelea kuwa daraja muhimu la maelewano nchini Tanzania na katika kanda za Afrika Mashariki na Kati. Ukuaji huu unathibitishwa na namna Kiswahili kinavyofundishwa katika vyuo vikuu barani Afrika, Ulaya, Asia, na Amerika, huku ikiwa ni lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.

Kutokana na umuhimu huo, Serikali ya Tanzania imetangaza mikakati thabiti ya kuimarisha lugha kupitia ujenzi wa maarifa, diplomasia ya kitamaduni, na kuandaa Atlasi ya Kitaifa ya Lugha-Mama za Tanzania. 

Aidha, Waziri Makonda alibainisha kuwa vijana si warithi wa lugha pekee, bali ni wabunifu wanaotumia teknolojia na majukwaa ya kidijitali kukuza Kiswahili katika tasnia za muziki, filamu, na utafiti. Serikali inatarajia kuendelea kushirikiana kwa karibu na UNESCO ili kuhakikisha wingilugha unakuwa nguzo ya ujumuishaji na maendeleo endelevu.

Kama sehemu ya utekelezaji wa azma hiyo, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuandaliwa kwa Kongamano la Kiswahili la Kimataifa litakalofanyika nchini Ufaransa kuanzia tarehe 27 hadi 30 Aprili 2026. 

Kongamano hilo linalenga kuenzi mchango wa UNESCO katika ukuzaji wa lugha hiyo na limetoa mwaliko kwa viongozi na wadau mbalimbali kushiriki. Akihitimisha, Waziri Makonda amesisitiza umuhimu wa kulinda lugha-mama ili kujenga mustakabali jumuishi wenye amani kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments