KUFANIKISHA AJIRA WAZIRI SANGU AVITAKA VYAMA VYA WAFANYAKAZI KUACHA MIGOGORO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amevitaka vyama vya wafanyakazi, waajiri pamoja na mashirikisho yao kote nchini kuachana na migogoro isiyo ya lazima na badala yake kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili ili kuimarisha ajira nchini.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na viongozi wa sekta hizo, Sangu amesisitiza kuwa lengo la kuanzishwa kwa vyama hivyo si kushindana wala kushutumiana, bali ni kulinda ustawi na kuhakikisha maisha bora kwa wafanyakazi wa Tanzania.
Waziri Sangu ametoa onyo dhidi ya tabia ya baadhi ya vyama kutumia majukwaa ya habari kushambuliana au kushushiana hadhi, jambo ambalo amesema halisaidii mfanyakazi bali linadhoofisha mshikamano.
Alibainisha kuwa serikali ilisajili vyama hivyo kisheria ili viwe daraja kati ya mwajiri na mwajiriwa, na si kuwa mahasimu. Amewataka viongozi hao kutoka katika malumbano na kurejea kwenye misingi ya majadiliano ya kijamii ili kutembea na azma ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuleta maendeleo na tija mahali pa kazi.
Kauli hiyo imeungwa mkono na wadau wa sekta ya ajira ambao wamebainisha kuwa kashfa na malumbano yanashusha hadhi ya viongozi wa wafanyakazi mbele ya jamii na serikali. Wadau hao wamesisitiza kuwa ili viongozi waweze kushawishi mabadiliko ya sera, ni lazima waonyeshe ukomavu na weledi kwenye meza za majadiliano ya utatu. Waliongeza kuwa migogoro ya vyama inawapa waajiri mwanya wa kupuuza maslahi ya wafanyakazi, hivyo kuna haja ya kuunganisha nguvu ili kuwa na sauti moja yenye mamlaka.
Aidha, jamii imewashauri viongozi hao wa vyama vya wafanyakazi kujikita kwenye mambo ya msingi yanayomgusa mfanyakazi wa hali ya chini, ikiwemo kima cha chini cha mshahara, makato makubwa ya kodi (PAYE), na ucheleweshaji wa mafao ya kustaafu,badala ya kupoteza muda kwenye vyombo vya habari kwa siasa za majitaka.
Post a Comment