TANZANIA YASAKA WABIA WA KIMKAKATI INDIA KUIMARISHA USALAMA WA NISHATI



Serikali ya Tanzania imeweka wazi dhamira yake ya kuifanya nchi kuwa kitovu cha nishati barani Afrika kwa kuvutia wawekezaji wa kimataifa wenye teknolojia ya kisasa na mitaji mikubwa. 

Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba,  leo Januari 27, ameshiriki ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Nishati nchini India yanayofanyika katika Jimbo la Goa. Hatua hii inalenga kuimarisha diplomasia ya nishati na kubainisha fursa za uwekezaji zilizopo nchini ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa nishati endelevu.

Katika maadhimisho hayo yaliyofunguliwa na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ujumbe wa Tanzania ulihusisha wataalamu kutoka taasisi za EWURA, TPDC, na PURA kwa lengo la kutafuta wabia watakaosaidia katika mageuzi ya nishati safi. 

Mheshimiwa Makamba amebainisha kuwa ushiriki wa Tanzania unalenga kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kusimamia rasilimali za nishati, hususan katika kipindi hiki ambacho dunia inahama kuelekea matumizi ya nishati zisizochafua mazingira.

Ingawa Tanzania imepata mafanikio makubwa kupitia miradi ya kitaifa kama Bwawa la Mwalimu Nyerere, serikali inaendelea kusisitiza umuhimu wa kuwa na vyanzo mchanganyiko vya nishati ili kuhakikisha usalama wa nishati wakati wote. Uwekezaji unaotafutwa unajikita katika nishati jadidifu kama jua na upepo, pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya gesi asilia ambayo ni muhimu katika kuchochea kasi ya maendeleo ya viwanda na kutoa fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi.

Mkakati huu wa serikali unatarajiwa kuleta tija kubwa kwa vijana wa Kitanzania kupitia upatikanaji wa ajira za kiufundi na uhamishaji wa teknolojia kutoka kwa mataifa yaliyoendelea kama India. Aidha, kuimarika kwa sekta ya nishati kutaongeza uwezo wa nchi kushiriki katika biashara ya kimataifa na kusaidia katika juhudi za kitaifa za kulinda mazingira kwa kupunguza utegemezi wa nishati zinazoharibu misitu.

No comments