SERIKALI YAZIPONGEZA JKCI NA ALMC KWA KUSOGEZA HUDUMA ZA MOYO KASKAZINI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa pongezi za kipekee kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) Selian kwa ushirikiano wao uliosaidia kusogeza huduma za kibingwa za moyo karibu na wananchi wa Kanda ya Kaskazini.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi mkoani Arusha hapo jana, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha huduma za ubingwa wa juu zinawafikia wananchi mahali walipo.
Mhe. Waziri Mchengerwa alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti unaolenga kuimarisha huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa.
Alisisitiza kuwa magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, sukari na saratani bado ni changamoto kubwa nchini, hivyo akawasihi wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini matatizo mapema.
Katika ziara hiyo, Waziri aliwahimiza wakazi wa Arusha na mikoa jirani kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (UHI) akieleza kuwa ndiyo nyenzo muhimu ya kulinda familia dhidi ya gharama kubwa za matibabu, hasa yale ya muda mrefu na kibingwa.
Aidha, Waziri alipongeza kuanzishwa kwa kituo cha ‘Sports Cardiology Centre’ katika hospitali ya ALMC-Selian ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya AFCON 2027, akibainisha kuwa kituo hicho ni fursa kwa Tanzania kuonesha uwezo wake katika huduma za afya na kuimarisha ajenda ya tiba utalii.
Takwimu za ushirikiano huo tangu mwezi Novemba 2025 zinaonesha mafanikio makubwa, ambapo jumla ya wagonjwa 11,051 wamepata huduma za kibingwa huku wagonjwa 482 wakilazwa kwa matibabu zaidi.
Vilevile, upasuaji mkubwa na mdogo umefanyika kwa wagonjwa 1,533 na wengine 1,297 wamepatiwa huduma za utengemao. Serikali imeahidi kuendelea kuboresha miundombinu ikiwemo vyumba vya upasuaji na kuongeza vifaa vya kisasa kama MRI na CT Scan.
Mwishoni mwa ziara yake, Mhe. Mchengerwa alitoa wito kwa wawekezaji, hususan wa mkoa wa Arusha, kuwekeza katika viwanda vya dawa na vifaa tiba. Alisema kuwa uzalishaji wa ndani utasaidia kupunguza gharama za uagizaji kutoka nje na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma bora nchini. Taarifa hiyo ilitiwa saini na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, John Mapepele.

Post a Comment