SERIKALI YASISITIZA VIWANDA VINAVYOMALIZA KERO ZA MASOKO KWA WAKULIMA NA WAFUGAJI



Serikali ya Awamu ya Sita imebainisha kuwa mwelekeo wake wa sasa katika uwekezaji ni kutoa kipaumbele kwa viwanda vinavyogusa maisha ya wananchi wa hali ya chini kwa kutoa ajira na masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo na mifugo.

Hayo yamesemwa  Januari 9, 2026, na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, wakati akitembelea viwanda mbalimbali mkoani Shinyanga kujionea shughuli za uzalishaji na mchango wa wawekezaji wazalendo.

Dkt. Chaya ameeleza kuwa Serikali inahitaji wawekezaji ambao uwekezaji wao unajibu kero za muda mrefu za wananchi vijijini na mijini.

“Tanzania ina idadi kubwa ya wakulima na wafugaji, lakini changamoto kubwa imekuwa ni masoko ya uhakika na viwanda vya kuchakata mazao hayo. Serikali inawatafuta na kuwahamasisha wawekezaji kama Jambo Group kwa sababu uwekezaji wao unawagusa wananchi moja kwa moja kwa kununua malighafi kutoka kwao,” amesema Dkt. Chaya.

Ameongeza kuwa viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao nchini ni nguzo kuu ya kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.

Ajira Elfu 11: Mfano wa Kuigwa 

Katika ziara hiyo kwenye Kiwanda cha Jambo Group of Companies, Naibu Waziri amemwaga sifa kwa mwekezaji huyo mzalendo kwa kutengeneza fursa za kiuchumi kwa kundi kubwa la Watanzania. Takwimu zinaonyesha kampuni hiyo imefanikiwa kutoa ajira kwa zaidi ya watu 1,000 wa kudumu na takribani 10,000 wa muda, wengi wao wakiwa ni vijana na wanawake.

Dkt. Chaya amewataka wawekezaji wengine wa ndani kuiga mfano huo wa kuwekeza kwenye bidhaa za matumizi ya kila siku (FMCG) ambazo zina soko pana na zinachochea uzalishaji wa malighafi kuanzia ngazi ya shamba.

Ili kuhakikisha uwekezaji huu unaendelea kushamiri, Dkt. Chaya amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu na kuondoa vikwazo vya kibiashara ili kuvutia mitaji zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jambo Group, Khamis Salum, amesema kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa ni za kiwango cha kimataifa kwa kutumia mitambo ya kisasa  .

Mbali na Jambo Group, Dkt. Chaya alitembelea pia kiwanda cha East African Spirits (T) Limited (EASTL), akihimiza uzalendo na uaminifu katika kulipa kodi ili kuiwezesha Serikali kuendelea kutoa huduma bora za kijamii.

No comments