SERIKALI YAIMARISHA HAKI YA FARAGHA KWA KILA MTANZANIA





Serikali imetoa msisitizo mkali kuhusu umuhimu wa ulinzi wa taarifa binafsi kama nguzo muhimu ya usalama wa raia na ustawi wa uchumi wa kidijitali nchini. 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amezitaka taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya au kuchakata taarifa za watu kuhakikisha zinajisajili katika Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ndani ya muda uliopangwa.

Akifunga mafunzo ya Maafisa wa Ulinzi wa Taarifa hivi karibuni, Waziri Kairuki ametangaza kuwa Serikali imeongeza muda wa miezi mitatu, kuanzia Januari 8 hadi Aprili 8, 2026, ili kutoa fursa ya mwisho kwa wadau wote kujisajili kwa hiari kwa mujibu wa Sheria.

Waziri Kairuki ameielekeza Tume ya PDPC kuanza maandalizi ya ukaguzi wa nchi nzima utakaofanyika mara baada ya tarehe ya ukomo kupita. Ukaguzi huo utahusisha:Taasisi za Umma na Wizara,Kampuni binafsi (zikiwemo za simu, mabenki, na bima) na Watu binafsi wote wanaojishughulisha na ukusanyaji au uhifadhi wa data.

“Serikali imetoa kipindi hiki cha nyongeza ili kutoa fursa ya mwisho. Baada ya hapo, ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria utaanza rasmi kwa kila taasisi na kampuni inayohusika na taarifa za wananchi,” alisema Mhe. Kairuki.

Hatua hii ya Serikali inalenga kulinda Haki ya Faragha ya kila Mtanzania, kuzuia matumizi mabaya ya taarifa binafsi, na kuimarisha usalama wa mtandao. Katika ulimwengu wa sasa, matumizi sahihi ya data yanatajwa kuwa chachu ya maendeleo kwani yanajenga uaminifu kati ya mtoa huduma na mteja, jambo ambalo ni muhimu kwa ukuaji wa biashara na huduma za kijamii.

Moja ya faida kubwa ya ulinzi wa Taarifa ni kuzuia wahalifu kuzitumia vibaya kwa wizi au utapeli.Aidha Taasisi zinapaswa kuwajibika kwa namna zinavyotumia taarifa za wananchi walizopewa na kuvutia Uwekezaji: Wawekezaji wa kimataifa hupendelea mataifa yenye sheria madhubuti za ulinzi wa data na taarifa binafsi.

Wito huu ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha kuwa mageuzi ya kidijitali nchini yanaenda sambamba na usalama wa raia na mali zao, huku msisitizo ukiwekwa katika matumizi ya teknolojia kwa ajili ya kuboresha ustawi wa taifa.

No comments