SEKTA YA UCHUKUZI YAPANDA CHATI PATO LA TAIFA
MCHANGO wa Sekta ya Uchukuzi katika Pato la Taifa umezidi kuimarika baada ya kupanda kutoka asilimia 7.2 mwaka 2023 hadi asilimia 7.5 mwaka 2024.
Hayo yamebainishwa na Makamu wa Rais, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la VIP katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA).
Alisema kasi ya ukuaji wa sekta hiyo sasa imefikia wastani wa asilimia 5.4, jambo linalotoa matumaini makubwa kwa uchumi wa nchi.
Dkt. Nchimbi alibainisha kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya uwepo wa sera nzuri za uwekezaji, amani na utulivu uliopo nchini, ambavyo vimevutia wawekezaji na washirika wa maendeleo. Aliongeza kuwa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuimarisha sekta hiyo ili iwe kichocheo kikubwa cha kukusanya mapato ya Serikali yatakayotumika kugharamia huduma nyingine za kijamii na maendeleo ya Taifa.
Dkt. Nchimbi alisema uwekezaji mkubwa unaofanywa kwenye reli ya SGR kuelekea mikoa ya kanda ya ziwa na nchi jirani ya Burundi, uboreshaji wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, pamoja na kuimarisha Shirika la Ndege (ATCL), unalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara (Hub) barani Afrika.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema Wizara yake inaendelea na hatua za upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vipya vya ndege katika maeneo ya kimkakati ya Serengeti, Kagera na Njombe ili kuchochea utalii na biashara.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Abdul Mombokaleo, alieleza kuwa jengo hilo la VIP limejengwa ili kuimarisha taswira ya nchi na kutoa huduma za daraja la kwanza kwa wageni mashuhuri wanaoingia nchini, hatua inayosaidia kuitangaza Tanzania kama nchi salama na yenye fursa pana za kiuchumi.









Post a Comment