SAYANSI NA TEKNOLOJIA: DARAJA LA TANZANIA KUELEKEA UCHUMI WA KIJANI NA DIRA 2050
Katika viwanja vya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST) jijini Arusha, mwangaza mpya wa maendeleo umeanza kumulika mustakabali wa Tanzania kupitia ushirikiano wa kimkakati na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Shigeki Komatsubara, ameweka wazi kuwa ufunguo wa mabadiliko chanya ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania upo katika kuunganisha ubora wa kitaaluma na suluhisho halisi zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja.
Komatsubara, akizungumza baada ya kutembelea taasisi hiyo Januari 26, amesisitiza kuwa dhamira ya kukuza viongozi wa baadaye na kuwawezesha wabunifu chipukizi inaendana na malengo ya kimataifa ya kuwekeza katika vipaji ili kuandaa maendeleo endelevu.
Mwakilishi huyo wa kimataifa ameeleza kuvutiwa kwake na msisitizo uliowekwa katika utafiti na ukuzaji wa vipaji vya vijana, akitaja uwepo wa maabara za kisasa za teknolojia ya kidijitali na akili unde, pamoja na umiliki wa kompyuta kubwa tatu za kisasa, kama kielelezo tosha cha uwezo wa juu wa Tanzania katika kuleta suluhisho za kiteknolojia.
Kwa mtazamo wa UNDP, sayansi na ubunifu si anasa, bali ni nguzo kuu zinazopaswa kuchochea maendeleo ya nchi, jambo linaloungana na juhudi pana za Serikali ya Awamu ya Sita ya kuandaa nguvukazi shindani kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo, Profesa Maulilio Kipanyula, amebainisha kuwa ushirikiano huu utajikita katika maeneo ya kipaumbele kama vile maabara za ubunifu, mabadiliko ya kidijitali, na kilimo mahiri kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi. Moja ya mipango kabambe ni uchumi wa kijani unaolenga kubadilisha taka kuwa fursa za kiuchumi, hatua itakayosaidia nchi kupata mafanikio ya kijani, ikiwemo juhudi za upandaji miti ambapo takwimu zinaonyesha jumla ya miti 113,199,000 imepandwa kuimarisha ikolojia yetu. Huu ni muendelezo wa mkakati wa dhahabu ambapo sayansi inatumika kutatua changamoto za kijamii huku ikitengeneza fursa za ajira kwa vijana.
Tanzania inapita katika mapinduzi ya ujuzi ambapo sayansi, teknolojia, na ubunifu ndizo injini kuu zinazoendesha taifa kuelekea uchumi imara na shindani. Kwa kuunganisha nguvu kati ya wasomi, mashirika ya kimataifa kama UNDP, na Serikali, nchi yetu inajenga msingi wa maendeleo usiotetereka ambao utahakikisha kila kijana wa Kitanzania anakuwa na utaalamu wa kutosha kuandika historia mpya ifikapo mwaka 2050.

Post a Comment