ODEMBA AUPIGA MWINGI MIONDOKO YA KIMATAIFA
Kama ulikuwa hujui maana ya "kustandout," basi malkia wa mitindo wa kimataifa kutoka Bongo, Miriam Odemba, ametoa darasa la bure mjini Paris!
Katika ufunguzi wa wiki ya mitindo ya kijanja zaidi duniani, Haute Couture Fashion Week, Odemba ameonyesha kuwa "old is gold" lakini "fashion is forever."
Akiwa anakata mitaa na miondoko ya kipekee kwenye runway, Odemba aliwafanya waliohudhuria washikwe na butwaa huku Paris yote ikishuhudia utofauti na ubunifu uliopitiliza.
Maonyesho haya yaliyoanza Januari 23 hadi 29, si mchezo! Paris imekuwa kitovu cha dunia ikikutanisha ufundi wa kisasa kutoka Madagascar, Ukraine, Urusi na kwingineko.Lakini Odemba wetu hakupita kinyonge; alisimama bega kwa bega na wabunifu wakubwa kama Christian Dior, Schiaparelli, na mbunifu hatari wa Cameroon, Imane Ayissi. Odemba ameweka wazi kuwa yeye yupo hapo kumuunga mkono mbunifu Victorine Muller wa Strasbourg, akichanganya uzoefu wake wa ukongwe na damu changa ya wabunifu chipukizi.
Sauti ya Mitindo: Kutoka Dar hadi Paris
Odemba si mwanamitindo tu wa kutembea jukwaani; yeye ni mwanamke wa mipango! Kupitia jukwaa lake la Sauti ya Mitindo, ambalo toleo lake la mwisho lilifanyika pale Dar es Salaam mwaka jana, Odemba sasa anaipeleka chapa ya Kiafrika katika soko la kimataifa kwa kasi ya 5G. Jukwaa hili limeanza kuvuta hisia za dunia, na Paris imekuwa sehemu ya yeye kuunganisha doti.
"Uwepo wangu hapa umeniunganisha na vipaji chipukizi ambavyo vimeikubali Tanzania," alisema Odemba kwa pozi la kishua. Ameongeza kuwa anatamani kuona toleo lijalo la Sauti ya Mitindo likileta mwingiliano wa kidunia, huku wabunifu wa Afrika Mashariki wakipanda lifti ya kimataifa kupitia ushirikiano wa dunia.
Dira ya 2050 na Diplomasia ya Urembo
Ubunifu huu wa Odemba unaendana kabisa na kasi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuifungua Tanzania kote duniani. Wakati serikali ikipambana na diplomasia ya uchumi kupitia viwanda na ajira, Odemba anapambana upande wa urembo na ubunifu, akihakikisha nguvukazi ya Kitanzania inaonekana kwenye majarida ya Vogue na Elle.

Post a Comment