RAIS WA CAF AIMWAGIA SIFA TANZANIA: ARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA AFCON 2027
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe, ameimwagia sifa Serikali ya Tanzania kwa hatua kubwa na jitihada za dhati zinazochukuliwa katika maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Motsepe ametoa kauli hiyo jijini Rabat, Morocco, wakati akipokea ujumbe maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliowasilishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda.
Katika mazungumzo hayo, Motsepe amepongeza uongozi wa Rais Samia kwa namna unavyowekeza kwenye miundombinu ya michezo, jambo ambalo si tu litafanikisha AFCON 2027.
Katika mazungumzo hayo Rais Motsepe ametangaza kuwa CAF itatuma timu ya wataalamu nchini Tanzania kwa ajili ya kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa soka kufanikisha malengo la A|fcon 2027.
Amesema lengo la timu hiyo ni kutoa mwongozo wa kitaalamu ili kuhakikisha Tanzania inafikia viwango vya kimataifa vinavyohitajika kwa ajili ya AFCON 2027, ambayo kwa mara ya kwanza inatarajiwa kushirikisha timu 25 badala ya 24.
Waziri Paul Makonda, akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa, amemhakikishia Rais huyo wa CAF kuwa Rais Samia amedhamiria kwa dhati kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha soka barani Afrika.
Waziri Makonda amesisitiza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika ujenzi na ukarabati wa viwanja na kuomba ushirikiano wa kimkakati kutoka CAF ili mipango ya Serikali ifanikiwe kwa asilimia mia moja.
Hatua hii inaashiria kuimarika kwa diplomasia ya michezo nchini Tanzania. Kauli ya Motsepe inatoa "baraka za kitalaamu" kwa Tanzania na inathibitisha kuwa ujenzi wa miundombinu unaoendelea mikoani (kama vile Arusha na Dar es Salaam) unafuatiliwa kwa karibu na mamlaka za juu za soka Afrika. Hii inaleta matumaini makubwa kwa mashabiki wa soka na wadau wa maendeleo ya vijana kupitia michezo nchini.

Post a Comment