ARUSHA YAIKALISHA DUNIA: CNN YAITAJA KUWA YA KWANZA KIUTALII 2026





JIJI la Arusha, ambalo ni kitovu cha utalii nchini Tanzania, limepata shavu jingine la kimataifa baada ya Kituo cha Habari cha CNN (CNN Travel) kuliainisha kama moja ya maeneo bora zaidi duniani ya kutembelea kwa mwaka 2026.

Katika ripoti yake maalum iliyochapishwa Desemba 31, 2025, CNN imeiweka Arusha kwenye rada za wasafiri wa kimataifa, ikivutiwa na mchanganyiko wa urembo wa asili, utajiri wa kitamaduni, na uzoefu wa kipekee wa safari (safari experience) ambao haupatikani kwingineko duniani.

CNN Travel imeielezea Arusha kama "lango la dhahabu" la kuelekea kwenye vivutio vikubwa zaidi Afrika. Ripoti hiyo imebainisha kuwa Arusha imezungukwa na maajabu kama Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kreta ya Ngorongoro, Tarangire, na Ziwa Manyara, huku ikiwa ni kambi kuu kuelekea kilele cha Mlima Kilimanjaro.

"Chini ya Mlima Meru unaovutia sana kuna Jiji la Arusha... mara nyingi ni lango la matukio mengine makubwa, lakini lenyewe lina urembo wa kipekee unaostahili kuonekana," ilieleza sehemu ya makala hiyo ya CNN.

Uchambuzi wa CNN umekwenda mbali zaidi na kuangazia Hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA) kama kivutio adhimu. Wasafiri wameshauriwa kutembelea hifadhi hiyo ili kujionea twiga na tembo wakizurura kwenye miteremko ya Mlima Meru, pamoja na maelfu ya ndege aina ya korongo wanaopamba Maziwa ya Momella.

Mandhari ya misitu mirefu na mazingira ya milimani yamefanya hifadhi hiyo kuanza kushindana kwa karibu na mbuga nyingine maarufu katika mzunguko wa Kaskazini.

Tanzania Yatikisa Mataifa Makubwa

Katika orodha hiyo ya maeneo bora ya kutembelea mwaka 2026, Arusha imekaa meza moja na maeneo mengine maarufu duniani kama:

Santa Monica (California, Marekani)

Kanazawa (Japan)

Adelaide (Australia)

Aragon (Hispania)

Devon (Uingereza)

Hatua hii imetafsiriwa na wachambuzi wa utalii nchini kama matunda ya kampeni endelevu za kuitangaza Tanzania kimataifa, zilizochochewa na filamu ya The Royal Tour na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha miundombinu ya usafiri , huduma kwa wageni na amani.

Kutajwa huku kwa Arusha kunategemewa kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa (International arrivals) mwaka huu, jambo litakalochochea biashara za hoteli, miongozo ya watalii (Tour Guides), na soko la bidhaa za asili, hivyo kuimarisha kipato cha wananchi mkoani hapa na nchi kwa ujumla.

No comments