UBUNIFU WA "SMART CHAJA" WAANGAZIA FURSA ZA VIJANA KATIKA MAZINGIRA YA AMANI
Katika hali inayoshiria kukomaa kwa fikra za kimaendeleo miongoni mwa vijana, mbunifu Thomas Ryoba amezindua huduma ya vituo vya kukodi kuchaji simu iitwayo “Smart Chaja,” mfumo unaomwezesha mteja kukodi power bank kupitia programu tumizi ya simu pindi anapopata dharura.
Ryoba amesisitiza kuwa huduma hiyo itapatikana katika maeneo rasmi kama ofisi, hospitali, na kumbi za starehe, huku akiwahimiza vijana wenzake kuchangamkia fursa za ubunifu ili kujipatia kipato na kufikia ndoto zao.
Hata hivyo, wadau wa maendeleo wamebainisha kuwa ubunifu kama huu wa Ryoba unahitaji mazingira tulivu na salama ili uweze kustawi na kuvutia wateja.
Maoni ya wananchi mtandaoni yamepongeza hatua hiyo kama "akili kubwa," yakisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia teknolojia kujenga uchumi badala ya kuitumia kama chombo cha kuvuruga utulivu. Amani imetajwa kuwa nguzo muhimu inayowezesha sekta binafsi na wabunifu wadogo kukua na kuchangia katika malengo ya serikali ya kukuza viwanda na ajira.
Wananchi wamehimizwa kulinda amani ili kutoa nafasi kwa wabunifu hawa kufanya kazi bila hofu ya uharibifu wa mali kama ilivyowahi kutokea mnamo Oktoba 29, ambapo baadhi ya makampuni yalichomwa moto wakati wa vurugu.
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama ni shwari, jambo linalotoa fursa kwa biashara na ubunifu mpya kama wa "Smart Chaja" kuendelea msimu huu wa sikukuu.

Post a Comment