Shilingi bilioni 57 kujenga Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Anga
Serikali imewekeza jumla ya shilingi bilioni 57 kujenga Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Anga katika Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) kilichopo Mabibo, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua majengo na vifaa vya kisasa vya kituo hicho, akibainisha kuwa uwekezaji huo unalenga kuwawezesha Watanzania kupata elimu bora ya anga kwa gharama nafuu ikilinganishwa na masomo hayo nje ya nchi.
Prof. Mbarawa amesema kukamilika kwa kituo hicho kutawawezesha vijana wengi wa Kitanzania kusomea fani za anga nchini na kuongeza idadi ya wataalamu wazawa katika sekta hiyo muhimu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha NIT, Mhandisi Prosper Mgaya, amesema jumla ya wanafunzi 100 tayari wamehitimu katika fani za urubani, wahudumu wa ndani ya ndege na uhandisi wa matengenezo ya ndege, huku idadi ya wanaojiunga na kozi hizo ikiendelea kuongezeka.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Profesa Ulingeta Bamba, amesema elimu inayotolewa katika kituo hicho inatambulika kimataifa, na amewahimiza vijana kuchangamkia fursa ya kupata mafunzo ya anga nchini.
Post a Comment