Msiwasikilize wapotoshaji huu ndio ukweli ,TAZARA Mpya ni Muhimili wa Mapato



Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa uboreshaji wa reli ya TAZARA kupitia mkataba wa kihistoria kati ya Tanzania, Zambia, na China, si tu utaleta mapinduzi ya kiuchumi, bali utaifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango kuu lisiloweza kuepukika barani Afrika.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amefafanua kuwa uwekezaji huo wa Dola za Marekani Bilioni 1.4 (zaidi ya Shilingi Trilioni 3.4) unaolenga kuifufua reli hiyo, utakuwa nguzo imara ya mapato ya nchi hata mbele ya ushindani wa korido mpya kama ile ya Lobito nchini Angola.

Bw. Msigwa amewataka Watanzania kupuuza upotoshaji unaofanywa kwenye mitandao, akisisitiza kuwa TAZARA inakwenda kuwa mhimili wa biashara ya madini adimu duniani (rare earth elements) na kichocheo cha viwanda, huku ikihakikisha Bandari ya Dar es Salaam inabaki kuwa kitovu cha biashara Kusini mwa Afrika.

Lango la Bandari ya Dar es Salaam Kwenda Nchi Jirani

Umuhimu wa TAZARA upo kwenye uwezo wake wa kipekee wa kuunganisha Bandari ya Dar es Salaam na mtandao wa reli wa Cape Gauge wenye urefu wa zaidi ya kilometa 50,000 barani Afrika. Huu ni ukanda unaounganisha mataifa mengi ya SADC, na kuifanya TAZARA kuwa njia fupi na yenye gharama nafuu zaidi kusafirisha mizigo mizito ikiwamo madini kama Cobalt, shaba, chuma, na makaa ya mawe kutoka Zambia, DRC, na kusini mwa Tanzania . Aidha mazao ya kilimo  kutoka maeneo ya Kusini yataweza kusafirishwa na kufikishwa sokoni kirahisi.

Ngao Dhidi ya Korido ya Lobito

Hata kama Korido ya Lobito (inayounganisha DRC/Zambia na Bahari ya Atlantiki) itakamilika, TAZARA itabaki kuwa mhimili imara wa mapato kwa Tanzania. Hii ni kwa sababu ya kuwepo kwa Kidatu Transshipment Hub. Ujenzi wa kituo hiki utaunganisha reli ya kati (MGR) na TAZARA (Cape Gauge), hali itakayofanya mizigo kutoka pande zote za Tanzania na nchi jirani kukutana na kuelekea Bandari ya Dar es Salaam kwa urahisi zaidi kuliko kuelekea magharibi.

Manufaa mengine ni mapato ya uhakika: Badala ya Serikali kutumia Shilingi Bilioni 28 kila mwaka kugharamia uendeshaji, sasa kampuni ya CCECC itailipa Serikali Dola Milioni 30 (Shilingi Bilioni 75) kila mwaka kama ada ya uendeshaji kwa miaka 30, huku miundombinu ikibaki kuwa mali ya nchi.

Diplomasia ya Rais Samia Yazaa Matunda

Mafanikio haya ni matokeo ya kazi kubwa ya kidiplomasia iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia mazungumzo yake na Rais wa China, Xi Jinping, na hotuba yake ya kihistoria katika Bunge la Zambia iliyochochea maridhiano ya nchi zote mbili kukubali uwekezaji huu.


No comments