Wakala wa Soka Akamatwa Baada ya Mchezaji 'Kutishiwa kwa Bunduki'
Wakala mmoja wa soka amekamatwa baada ya kudaiwa kumtishia mchezaji wa Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League) kwa bunduki.
Tukio hilo limeelezwa kutokea jijini London Septemba 6 huyo mwaka huu na kuleta fadhaa kubwa kwa mchezaji huyo ambaye hawezi kutajwa kisheria - alilazimika kukabiliana na kitisho hicho kwa fadhaa kubwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) katika taarifa yake ya Novemba 3 Klabu ya mchezaji huyo inafahamu kuhusu tukio hilo.
Katika mfumo wa sheria wa Uingereza, kuna kanuni na amri mbalimbali za mahakama zinazotumika kulinda utambulisho wa watu wanaohusika katika kesi wakiwemo waathiriwa. Hii inajulikana kama Amri za Kuzuia Utangazaji (Reporting Restrictions au Anonymity Orders).
Lengo kuu la sheria hizo ni kulinda faragha ya mhusika, kuzuia madhara zaidi, na kuhakikisha kuwa haki ya kusikilizwa inatendeka bila ushawishi au shinikizo kutoka kwa umma.
Kutokana na sheria hiyo imeelezwa kuwa kutaja jina la mchezaji huyo kunaweza kuongeza kiwewe alichopitia na kuathiri hali yake ya kiakili au maisha yake ya soka.
Lengo jingine la kutotatajwa kwa mchezaji huyo ni kuzuia kuathiri upelelezi wa polisi au kesi ya baadaye mahakamani, hasa kwa kuwapa umma maelezo ambayo hayakupaswa kutolewa.
Inadaiwa kwamba mwanaume mwingine pia alitishwa na kunyang'anywa kwa njia ya vitisho na mtu huyo huyo wakati wa tukio hilo. Hakuna majeraha yaliyoripotiwa katika matukio yote mawili.
Polisi waliitwa saa 23:14 BST (Saa za Uingereza) kufuatia ripoti kwamba mwanaume mmoja alikuwa ametishiwa kwa kutumia silaha ya moto.
Mshukiwa huyo, mwenye umri wa miaka 31, alikamatwa mnamo Septemba 8 kwa tuhuma za kumiliki silaha za moto kwa nia ovu, unyang'anyi wa vitisho (blackmail), na kuendesha gari bila leseni. Amepewa dhamana wakati upelelezi ukiendelea. Jeshi la Polisi la Metropolitan linaendelea kuchunguza tukio hilo.

Post a Comment