Watanzania waishio Marekani wamuunga mkono Rais Samia
Watanzania
wanaoishi Marekani wamejitokeza kwa wingi kuunga mkono Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku
wakilaani vikali uchochezi unaofanywa na mwanaharakati wa mtandaoni, Mange
Kimambi, wanaomtuhumu kutumia mitandao kujaribu kuichafua nchi na kupandikiza
chuki kwa Watanzania.
Kwenye mahojiano maalum na waandishi wetu
kupitia simu na majukwaa ya kijamii, Watanzania hao wametoa sauti moja ya
amani, mshikamano, na maendeleo wakisisitiza kuwa hakuna sababu yoyote ya
vurugu nchini Tanzania, ambayo kwa sasa inatajwa kuwa miongoni mwa nchi salama
na zenye uchumi imara barani Afrika.
Arnold Kaira, Mtanzania anayeishi Texas kwa
zaidi ya miaka 10, alisema kwa hasira: “Rais anafanya kazi kubwa ya maendeleo.
Tunaona upanuzi wa miundombinu, sera za uwekezaji na uchumi unaokua. Kwa nini
tutake kuvuruga haya yote? Huyu dada anayetaka machafuko achunguzwe, anaonekana
kutumika na maadui wa nchi yetu.”
Naye Bi. Maria Kapinga, mfanyabiashara kutoka
Washington DC, aliongeza: “Maandamano anayoyahamasisha Mange hayana msingi.
Tanzania inapiga hatua, barabara, viwanja vya ndege, elimu bure, huduma bora za
afya. Tunajivunia nchi yetu, siyo kuiharibu.”
Kwa upande wake, mwekezaji kutoka California,
Joseph Bamba, alisisitiza kuwa uchochezi huo ni tishio kwa uwekezaji: “Serikali
ya Rais Samia imeweka mazingira bora kwa wawekezaji. Tunaona ukuaji katika
sekta ya kilimo, utalii na uchumi wa buluu. Uchochezi huu ni hatari kwa
mustakabali wa maendeleo.”
Aidha, mwalimu na mfanyabiashara Bi. Lillian
Mushi kutoka New York, aliongeza: “Kama mama na mwalimu, ninaona juhudi kubwa
za Serikali katika elimu na afya. Mange anataka kuharibu haya yote. Sisi
Watanzania wa Marekani tunasema hapana amani kwanza, maendeleo mbele.”
Mwakilishi wa Ubalozi wa Tanzania Marekani
(ambaye hakutaka jina litajwe) alithibitisha kuwa siku ya maandamano
yaliyodaiwa kufanyika Oktoba 17, walijitokeza watu wachache tu, bila sapoti
yoyote kutoka jamii ya Watanzania walioko Marekani: “Watanzania wa hapa
wanaelewa kinachoendelea nyumbani. Wanashiriki kukuza picha chanya ya Tanzania,
siyo kuichafua.”

Post a Comment