Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Ndugu Wallace
Karia ametoa salamu za pongezi kwa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20
(Ngorongoro Heroes) na ile ya chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kwa kufanikiwa
kufuzu katika michezo yao iliyochezwa jana huko DR Congo na Burundi.
Ngorongoro Heroes
wamefanikiwa kusonga kwenye raundi ya pili ya kufuzu fainali za Africa za
Vijana chini ya miaka 20 zitakazochezwa Niger mwezi Novemba baada ya ushindi
wake wa penati 5-6 dhidi ya DR Congo baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya
bila kufungana kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa nchini
Tanzania wakati Serengeti Boys wenyewe wamefuzu hatua ya nusu fainali ya
mashindano ya Vijana ya Cecafa chini ya miaka 17 inayoendelea huko Burundi.
Rais wa TFF Ndugu Karia
amesema kufanya vizuri kwa timu hizo za vijana ni faraja kubwa kwa Tanzania na
inaonesha namna ambavyo TFF inaendelea kuwekeza kwenye soka la vijana.
Amesema Vijana hao wa
Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys wameonesha jitihada kubwa na wanastahili
pongezi kwa jitihada hizo pamoja na jitihada za mabenchi ya ufundi ya timu
hizo.
“Tumepokea matokeo ya Vijana
wetu wa Ngorongoro na Serengeti Boys kwa furaha kubwa kwasababu tumekuwa
tukihakikisha timu hizi zinapata maandalizi mazuri ambayo yanaonekana uwanjani
kwa kupata matokeo mazuri ambayo yanailetea sifa kubwa Tanzania kwa ujumla”
alisema Karia.
Aidha Rais wa TFF Ndugu Karia
amesema TFF itaendelea na jitihada kuzipatia maandalizi mazuri zaidi timu hizo
ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali yanayowakabili.
Amesema TFF inajivunia vijana
hao ambao wanaonesha mwanga mkubwa na amewaomba watu
mbalimbali,Taasisi,makampuni kuunga mkono jitihada za TFF na kuiga mfano wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojitokeza na kuisaidia Ngorongoro Heroes
katika safari yake ya kwenda DR Congo kwenye mchezo wa marudiano.
Amemalizia kwa kuwashukuru
wote wanaounga mkono jitihada za TFF kuendeleza mpira wa Tanzania huku
akiishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais John
Pombe Magufuli kwa kuunga mkono na ushirikiano wao kwa TFF.
No comments:
Post a Comment