YANGA kesho inakutana
na Singida United katika mchezo wa robo fainali wa Kombe la FA huku kila timu ikiwataka mashabiki wake kuondoa wasiwasi, kwani kila kitu
kipo poa.
Mechi hiyo
inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini kutokana na ubora wa
timu hizo, unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.
Katika kuonesha
kuwa Yanga wamepania kufanya kweli, timu hiyo iliamua kwenda kuweka kambi ya
takriban siku nne mkoani Morogoro kwa ajili ya mechi hiyo, ambapo jana
ilielezwa kuwa walianza safari ya kuifuata Singida.
Katibu Mkuu
wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa alisema kuwa timu hiyo imefanya
maandalizi ya kutosha kuelekea katika mechi hiyo na dhumuni ni kuhakikisha
wanaibuka na ushindi na kusonga mbele hivyo wanaingia mkoani humo wakiwa kamili
kwa ajili ya vita hiyo.
“Kikosi
kimejiandaa vya kutosha, kulikuwa na programu nyingi za kujipanga kwa ajili ya
mchezo huo, ambapo mambo yamekwenda vizuri na timu ikiwa kamili tangu kwenye
maandalizi Morogoro tayari kwa mchezo huo, ambao tunahitaji ushindi, tusonge
mbele na kufanikisha tunalolihitaji,” alisema Mkwasa.
Mbali na
ubora wa vikosi hivyo, lakini kutoshana nguvu kwa timu hizo mara mbili
zilipokutana msimu huu, imekuwa sababu kubwa ya kutaka kujua nani atachanga
karata zake vizuri safari hii kwa kumtoa mwenzake na kutinga nusu fainali ya
michuano hiyo, ambayo bingwa ataiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho
Afrika.
Katika mechi
hizo mbili za awali, ya kwanza ilikuwa ya Ligi Kuu, ambapo Singida
ililazimishwa suluhu katika uwanja wake wa nyumbani kabla ya kukutana tena
kwenye Kombe la Mapinduzi katika hatua ya makundi na matokeo yalikuwa sare ya
1-1.
Upande wa
pili, Mkwasa pia amezungumzia mipango inayoendelea katika kujiandaa kuwasoma
wapinzani wao Welayta Dicha kutoka Ethiopia watakaoumana nao April 7, mwaka huu
kuwania kufuzu kuingia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Tunaendelea
na maandalizi kama kawaida, tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunafanya
vizuri kwenye Shirikisho pia. Kocha Lwandamina (George) amekwenda Ethiopia
ikiwa ni sehemu ya kuwafahamu vizuri wapinzani wetu na hiki ni kitu cha kawaida
tu katika kutafuta ushindi, hufanyika duniani kote,” alifafanua Mkwasa.
Wakati Yanga
ikiyaeleza hayo, Kocha Mkuu wa Singida, Hans van Pluijm ametamba kuwa
wamejiandaa vya kutosha kuifunga Yanga huku akieleza jinsi gani anawafahamu
wapinzani wake hao.
“Naifahamu
Yanga, ni timu kubwa na yenye wachezaji wenye uzoefu wa hali ya juu na wameshiriki
michuano hii kwa muda sasa. Kwa kulitambua hilo pamoja na maandalizi mengi ya
kutosha tunayoyafanya kwa ajili ya mechi hiyo lakini nidhamu ya mchezo juu ya
wapinzani wetu ni suala la msingi.
“Tunahitaji
kuvuka kwenye hatua hii na kwenda nusu fainali tukiwa na lengo la kupata
mafanikio zaidi katika kombe hili ndiyo maana kumekuwa na maandalizi ya kutosha
kuhakikisha tunapata ushindi katika kila mchezo ulio mbele yetu,” alisema
Pluijm kocha wa zamani wa Yanga.
No comments:
Post a Comment