KAMATI ya
Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia kujihulisisha na soka maisha
Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura, baada ya kumkuta na hatia katika tuhuma
tatu zilizokuwa zinamkabili kwa mujibu wa Kifungu cha 73(1)(c) cha Kanuni za Maadili ya TFF
toleo la 2013.
Wambura
alifikishwa kwenye kamati ya maadili na sekretarieti ya TFF juzi kwa
makosa ya kupokea fedha za TFF kwa malipo yasiyo halali, kugushi barua na
kushusha hadhi ya taasisi hiyo hivyo pamoja na kufungiwa maisha kamati imeielekeza Sekretarieti, kwa
kupitia kifungu cha 6(3) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013, ilifikishe
suala hili katika vyombo vya dola ili vifanye uchunguzi.
Katika
suala hilo Kamati inakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Ukaguzi kuwa
waliokuwa viongozi wakuu wa TFF wakati malipo hayo yanafanyika, Jamal Malinzi
(Rais) na Celestine Mwesigwa (Katibu Mkuu) nao waunganishwe katika uchunguzi
huo.
Kamati ya maadili ilikutana juzi na kusikiliza shauri hilo
ambalo Wambura aliwakilishwa na wakili Emanuel Muganyizi kwani kisheria alikuwa
na hiari ya kufika kutoa utetezi huo kwa njia ya mdomo, kutuma kwa maandishi,
kuleta mashahidi au kutuma mwakilishi akiambatana na barua ya uwakilishi
Hukumu hiyo ilisomwa leo na Kaimu Ofisa habari wa TFF,
Cliford Ndimbo kwa mamlaka ya kamati hiyo akiwa na Mwenyekiti Wakili Hamidu
Mbwezeleni katika Ukumbi wa mikutano wa TFF
Baada ya kuelezwa mashtaka yanayomkabili
mteja wake, Wakili Muga aliiomba Kamati kuwa mteja wake anaomba kupewa muda wa
kupitia shauri hilo ili aandae utetezi, vielelezo, na mashahidi. Mara baada ya
kutoa ombi hilo Kamati ilimruhusu asubiri ili ipitie kabla ya kufanya uamuzi.
Baada ya majadiliano wajumbe walikubaliana kuwa suala hili si geni kwa Ndugu
Wambura; hivyo siyo kweli kuwa hana ufahamu nalo. Pia moja ya vielelezo
vilivyowasilishwa mbele ya Kamati ni utetezi wa maandishi wa Ndugu Wambura
kuhusiana na suala hilo ulioandikwa 4/12/2017. Hivyo Kamati ilijiridhisha kuwa
Ndugu Wambura anao ufahamu wa kutosha wa suala hilo na alikuwa na uwezo wa
kufika mbele ya Kamati ili kutoa maelezo ya ziada.
Kamati ilimjulisha Wakili Muga kuhusiana
na uamuzi huo na kumtaka aanze kujikita katika kujibu mashtaka yaliyowasilishwa
mbele yake. Hata hivyo Wakili Muga hakutaka kufanya hivyo na badala yake
aliomba apewe muda zaidi wa kuandaa utetezi, vielelezo, na mashahidi. Kamati
ilimkumbusha Wakili Muga kuwa wito wake ulijieleza vizuri hivyo ilikuwa ni
wajibu wake kumshauri mteja wake ipasavyo na kumsaidia katika kujibu mashtaka
yaliyofikishwa mbele yake. Baada ya maelezo hayo Kamati ilimuuliza Wakili Muga
kama yuko tayari kuendelea na shauri au vinginevyo na yeye akaridhia kuwa
shauri liendelee.
Baada ya makubaliano hayo, Wakili Muga
alipewa nafasi ya kujibu mashtaka matatu yanayomkabili mteja wake.
Shitaka la kwanza:
“Kupokea/kuchukua fedha
za Shirikisho (TFF) za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na
kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.”
Sekretarieti iliwasilisha ushahidi
unaoonyesha kuwa Ndugu Michael Richard Wambura alipokea malipo kutoka Chama cha
Miguu Tanzania (FAT) na baadaye TFF ikiwa ni marejesho ya mkopo ambao FAT
ilikopeswa dola la kimarekani $30,000 kutoka katika kampuni ya JEKC SYSTEMS
LIMITED kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka
2002. Mkataba wa deni hilo ulisainiwa na Ndugu Wambura akiwa Katibu Mkuu wa
FAT. Hata hivyo Kamati haikupata nyaraka wala kumbukumbu zozote zile
zinazoonyesha kuwa Ndugu Wambura alipata idhini ya kukopa kiasi hicho cha fedha
kutoka katika Kamati Tendaji ya FAT. Vilevile Kamati haikuona uthibitisho wa
kiasi hicho kupokelewa kwenye akaunti za FAT zaidi ya Mkataba ambao ulisainiwa
na Ndugu Wambura peke yake bila kuwa na shahidi mwingine kutoka FAT kinyume na
taratibu za kawaida za mikataba. Vile vile Kamati imeshangaa ni taratibu gani
zilitumika kwa taasisi kama FAT kuchukua mkopo mkubwa kama huo kwenye kwenye
kampuni hiyo badala ya taasisi za fedha kama vile benki ambazo ndizo
zinazojishughulisha na masuala hayo.
Sekretarieti iliwasilisha ushahidi
unaoonyesha kuwa Ndugu Wambura, kwa nyakati tofauti, alipokea jumla ya
sh.84,000,000.00 kutoka FAT na baadaye TFF kama marejesho ya mkopo kwa niaba ya
kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED. Hata hivyo Kamati haikupata uthibitisho wa
kisheria kutoka kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED unaomuidhinisha Bw. Wambura
kupokea malipo ya mkopo huo kwa niaba yake zaidi ya barua Kumb. Na.
JKC/CONT/TFF/2014 ya tarehe 13/1/2014 kutoka kwa kampuni hiyo. Hata hivyo barua
hiyo, licha ya kuandikwa miaka 10 baada ya Bw. Wambura kuchukua nusu ya mkopo
huo, haikuwahi kupokelewa TFF na wala haikidhi matakwa ya kisheria ambayo ni
kuwa na Power of Attorney iliyosajiliwa kwa Msajili wa Hati na Nyaraka.
Kulingana na ushahidi uliowasilishwa na
Sekretarieti malipo ya mkopo huo yalifanyika kwa awamu ambapo mara ya kwanza
Ndugu Wambura alilipwa $15,000 alizopokea tarehe 29/4/2004. Hata hivyo Kamati
ilibaini mapungufu katika fomu hiyo kwani maombi ya kulipwa fedha hiyo
yalitolewa na Ndugu Wambura na kuidhinishwa na yeye mwenyewe, kinyume na
taratibu za fedha.
Malipo hayo ya mkopo hayakufanyika kwa
kipindi cha miaka 10, chini ya Uongozi wa Ndugu Leodgar C. Tenga, mpaka
alipoondoka madarakani na kuingia uongozi mpya chini ya Ndugu Jamal Malinzi
ndipo yalipoanza kufanyika tena. Kamati inapata mashaka juu ya uhalali wa deni
na malipo hayo kwani hakukuwa na madai wala malalamiko yoyote yaliyowasilishwa
kudai au kukumbushia deni hilo kwa kipindi chote hicho. Katika hali ya kawaida
siyo rahisi kulipa deni hilo bila kujiridhisha uhalali wake.
Shitaka la pili
“Kughushi barua ya kuelekeza alipwe
malipo ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali
ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la
2013.”
Sekretarieti iliwasilisha nakala ya barua
ya tarehe 21/6/2016 kutoka kwa Bibi Irene W. Maganga ambaye ni mke
wa mmiliki wa kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED, Marehemu Enock Maganga na mmoja
wa wasimamizi wa mirathi ya marehemu walioteuliwa na Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Barua hiyo inakanusha kuwa kampuni hiyo haikuwahi kupokea malipo yoyote ya deni
hilo. Hii inaonyesha kuwa Ndugu Wambura hakuwahi kupewa mamlaka ya kupokea
fedha hizo na pia hakuwahi kuziwasilisha kwa wamiliki wa kampuni hiyo fedha
alizopokea kutoka FAT na TFF.
Kwa msingi huo hata uhalali wa barua Kumb. Na.
JKC/CONT/TFF/2014 ya tarehe 13/1/2014 kutoka kwa kampuni hiyo aliyoiwasilisha
kuonyesha kuwa ameidhinishwa kupokea malipo hayo unatia shaka. Ndugu Wambura
hajawahi kukanusha maelezo yaliyomo kwenye barua hiyo licha ya kupewa nafasi
akiwa Makamu wa Rais wa TFF.
Shitaka la tatu:
“Kufanya vitendo
vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba
ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015)”
Kamati
imejiridhisha bila shaka kuwa vitendo vya Ndugu Wambura vinashusha hadhi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF). Kitendo cha Ndugu Wambura kuiingiza FAT na
baadaye TFF katika mkopo wa $30,000 bila kufuata taratibu zozote ni ukiukwaji
mkubwa wa maadili. Vile vile kitendo hicho kimelipaka matope shirikisho hilo
mbele ya umma kwani mambo aliyoyafanya hayaakisi ukubwa na umuhimu wa taasisi
hiyo. Kwa nafasi yake ya Makamu wa Rais, Ndugu Wambura ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Fedha na Mipango, hivyo vitendo hivyo haviendani na hadhi na majukumu ya
nafasi yake hiyo.
HUKUMU
Kosa la kwanza:
Kulingana na kifungu cha 73(1) cha Kanuni
za Maadili ya TFF toleo la 2013, Ndugu Michael Richard Wambura, amefanya kosa
la kifisadi ambalo adhabu zake ni;
- (i) faini isiyopungua shilingi 10,000,000.
(ii)
kifungo cha cha kutojihusisha na mpira wa miguu kwa miaka isiyopungua 5
- Kama suala ni zito na limekuwa likijirudia rudia,
kifungo cha kutojihusisha na mpira wa miguu maisha.
Kosa
la pili:
Kwa
kosa la kughushi kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013,
kinatoa adhabu ya kifungo cha cha kutojihusisha na mpira wa miguu kwa miaka
isiyopungua 5.
Kosa
la tatu:
Kwa
kosa la kushusha hadhi ya Shirikisho ni kwenda kinyume na Katiba ya TFF
(kama ilivyorekebishwa 2015). Hili ni kosa la kimaadili ambalo adhabu zake
zinaenda sambamba na adhabu nyingine zinazotolewa na Kanuni za Maadili ya TFF
toleo la 2013.
Baada
ya kupitia shauri hili na kuridhika pasipo na shaka kuwa Ndugu Michael Richard
Wambura ametenda makosa hayo yote, Kamati imemfungia Ndugu Michael Richard
Wambura kifungo cha kutojihusisha na mpira wa miguu maisha. Adhabu hii
imetolewa kwa kuzingatia uzito wa kosa lake kwa mujibu wa Kifungu cha 73(1)(c)
cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.
Kwa
kuwa suala hili linahusisha masuala ya rushwa, Kamati inaielekeza Sekretarieti,
kwa kupitia kifungu cha 6(3) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013,
ilifikishe suala hili la Ndugu Michael Richard Wambura katika vyombo vya dola
ili vifanye uchunguzi. Aidha Kamati inakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya
Ukaguzi kuwa waliokuwa viongozi wakuu wa TFF wakati malipo hayo yanafanyika,
Ndugu Jamal Malinzi (Rais) na Ndugu Celestine Mwesigwa (Katibu Mkuu) nao
waunganishwe katika uchunguzi huo.
HITIMISHO
Kamati
haikupendezwa na taarifa zilizowasilishwa na Sekretarieti kuhusu juhudi
zilizofanywa na vyombo mbalimbali kuizuia isifanye kazi yake kwa mujibu wa
Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015) na Kanuni za Maadili ya
TFF toleo la 2013. Kamati inaviasa vyombo hivyo kutoingilia mambo ya mpira wa
miguu, hasa vyombo vya kimaamuzi, kwani athari zake zinaweza kuwa kubwa kwa
ustawi wa mpira wa miguu nchini.
No comments:
Post a Comment