Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Kidao
Wilfred (katikati) akitoa ufafanuzi kuhusu waamuzi wa kimataifa wa Tanzania
wanaotuhumiwa kwa rushwa katika mchezo wa klabu bingwa barani Afrika kati ya
Lydia ya Burundi na Rayon ya Rwanda. Kushoto ni Katibu Mkuu wa DRFA, Msanifu
Kondo na Kaimu Ofisa habari wa TFF, Clinford Ndimbo. (Picha na Rahel Pallangyo)
WAAMUZI wa Soka wanne wa
Kimataifa wa Tanzania wanatuhumiwa kwa rushwa na Shirikisho la soka Barani
Afrika (CAF) suala hilo limepelekwa kamati ya nidhamu ya CAF.
Akizungumza na waandishi wa
habari, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Kidao
Wilfred alisema walipata barua Februari
23 kutoka CAF kuwa mchezo wa mabingwa Afrika dhidi ya Rayon (Rwanda) na Lydia
(Burundi) ulikuwa na matatizo.
“Tuliambiwa tujieleze kwa
sababu waamuzi waliokwenda kuchezesha Mfaume Nassoro, Frank Komba, Soud Lila na
Israel Mujuni walitoka Tanzania,”
“Siku moja kabla ya mchezo
kulitokea na sintofahamu kwenye hoteli waliyofikia waamuzi na inasadikika viongozi wa Rayon walikutwa
kwenye chumba cha mmoja wa waamuzi wetu lakini siku hiyo hiyo kulitokea fujo
baina ya viongozi wa timu mgeni (Rayon) na viongozi wa Lydia ikalazimika polisi
kuingilia kati,” alisema Kidao.
Baada ya matukio hayo polisi
iliwashikilia viongozi wa timu mgeni na kamishna wa mchezo huo ambaye ni
Gradmoo Mzambi kutoka Zimbabwe alitoka baada ya kusikia kelele na ikaitaarifu
CAF kuhusu kilichotokea.
Kidao alisema Februari 27
waliaindikiwa tena barua na CAF kutaka maelezo ya tukio hilo yawe yamewafikia
kabla ya Machi 6 na wao ilibidi kufanya uchunguzi kabla ya kuiandikia CAF.
Anasema taarifa ya kamishna wa
mchezo huo ndio inaweza ikawasafisha au kuwahukumu kwa sababu kwenye hoteli
waliyofikia kulikuwa na CCTV kamera na imeambatanishwa kwenye ripoti ya kamishna.
“Jambo hili limepelekwa kwenye
kamati ya nidhamu ya CAF na bdio italitolea maamuzi lakini sekretarieti ya TFF
itakutana na kamati ya waamuzi ya Tanzania kujadiliana lakini hatuwezi kutoa
maamuzi hadi CAF walifanyie kazi,” alisema Kidao
Kidao anasema TFF inataka haki
itendeke hata kama waamuzi wetu watakuwa wamefanya makosa kwani ni jambo ambalo
halina twasira nzuri kwa maendeleo ya soka.
Katika mchezo huo wa klabu
bingwa barani Afrika Rayon ilifunga Lydia 1-0 na kufanikiwa kusonga mbele.
No comments:
Post a Comment