SIMBA kesho itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiikaribisha timu ya Al Masry ya
Misri katika mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika utakaoanza saa 12:00
jioni.
Wawakilishi
hao wa Tanzania wanaingia uwanjani wakiwa na ari ya ushindi ili kupunguza kazi
katika mchezo wa marudiano, kwani Waarabu wana tabia ya kucheza kwa kujihami
ugenini na nyumbani kushambulia sana.
Kocha wa
Simba, Mfaransa Pierre Lechantre alisema anaifahamu Al Masry na timu nyingine
za Misri kuwa ni timu zinazocheza soka la kujihami zikiwa ugenini, lakini
nyumbani wanashambulia hivyo watajitahidi kuhakikisha wanapata ushindi nyumbani
ili ugenini wawe na kazi nyepesi.
“Wachezaji
Emmanuel Okwi na John Bocco watakuwepo lakini sisemi tutaingia kwa staili gani
bali tutacheza kutafuta ushindi kwa sababu timu zinazotoka nchi za Kiarabu zina
tabia ya kucheza mchezo wa kujihami ugenini,” alisema Lechantre.
Naye nahodha
wa timu hiyo, John Bocco alisema matokeo ya sare ya 3-3 ya Ligi Kuu dhidi ya
Stand United yasiwatie hofu waje kwa wingi kuishangilia timu yao, kwani
wachezaji wanajua deni walilonalo kwao.
“Kocha
amefanya kazi yake na sisi wachezaji tumejiandaa kuhakikisha tunapata ushindi,
kwani ni muda mrefu Simba haijashiriki mashindano ya kimataifa hivyo mashabiki
waje kwa wingi kuisangilia timu yao,” alisema Bocco.
Wakati Simba
ikiongoza Ligi Kuu Tanzania Bara, wapinzani wao wanashika nafasi ya nne katika
ligi nchini Misri.
Kocha wa Al
Masry, Hossam Hassan atakuwa na kumbukumbu ya kipigo alichopata kutoka kwa
Simba wakati akichezea Zamaleck mwaka 2003 baada ya kufungwa bao 1-0 Dar es
Salaam na ugenini Simba ikafungwa bao 1-0 na kutolewa kwa penalti 3-2 baada ya
matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1.
Timu hiyo inamtegemea
mshambuliaji raia wa Burkina Faso Aristide Bance ambaye amegeuka gumzo hapa
nchini na kwenye mitandao ya kijamii.
Simba ilifuzu
hatua ya awali kwa kuiondoa Gendermarie ya Djibout kwa mabao 5-0 wakati
wapinzani wao Al Masry walifuzu kwa kuishinda Green Buffalo ya Zambia kwa mabao
5-2.
Kiingilio
katika mchezo huo VIP A ni Sh 20, 000, VIP B ni Sh 15,000 na mzunguko Sh 5,000.
Baada ya mchezo
wa huo wa leo, timu hizo zitarudiana siku 10 baadaye mjini Cairo, Misri na
mshindi wa jumla ataingia kwenye mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi kwa
kucheza na moja ya timu zilizotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu
zinazoingia hatua ya makundi Kombe la Shirikisho hupewa dola za Marekani
150,000 (zaidi ya Sh milioni 300), ambazo huongezeka kila timu inaposhinda na
kusonga mbele.
Bingwa wa Kombe
la Shirikisho hupata Dola za Kimarekani 625,000 (zaidi ya Sh bil 1.5), mshindi
wa pili wa Kundi hupata dola 239,000.
No comments:
Post a Comment