MABINGWA
watetezi wa Ligi Kuu Yanga, leo wamezidi kujiimarisha katika kutetea ubingwa
huo baada ya kushuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Majimaji.
Katika
mchezo huo uliochezwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Yanga ilitawala karibu
kila eneo katika vipindi vyote.
Yanga
ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 20 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti
na Pappy Tshishimbi.
Penalti hiyo
ilitolewa na mwamuzi Nassoro Mwinchui wa Pwani baada ya Mpoki Mwakinyuke wa
Majimaji kushika mpira kwa mkono akimzuia Obrey Shirwa kufunga wakati kipa wa
Majimaji Salehe Malande akiwa ameanguka.
Kutokana na
kosa hilo, mwamuzi alimuonesha Mwakinyuke kadi nyekundu.
Dakika tisa
baadaye, Chirwa aliiandikia Yanga bao la pili akiunganisha krosi ya Gadiel
Michael.
Dakika mbili
kabla ya kwenda mapumziko Emmanuel Martin alifunga bao la tatu kwa shuti kali
nje ya 18 lililotinga moja kwa moja wavuni.
Kipindi cha
pili kilianza kwa Majimaji kutaka kuresha bao na jitihada zao zilianza kuzaa
matunda baada ya kupata penalti katika dakika ya 56 na Marcel Bonavanture
kuukwamisha mpira wavuni.
Mwamuzi
Mwanchui alitoa penalti hiyo baada ya Saidi Makapu wa Yanga kushika mpira eneo
la hatari.
Tshishimbi
aliwainua tena mashabiki wa Yanga katika dakika ya 85 alipoandika bao la nne
kwa shuti kali karibu na 18 na kujaa wavuni.
Ushindi huo
umeifanya Yanga kufikisha pointi 37 nyuma ya kinara Simba iliyo kileleni kwa
Pointi 41.
Aidha,
matokeo hayo yamezidisha presha kwa Simba iliyo ugenini Shinyanga leo kucheza
dhidi ya Mwadui ambapo salama yake ni ushindi ili iendelee kujiimarisha.
No comments:
Post a Comment