MABINGWA
watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo wamepunguzwa kasi baada ya
kulazimishwa suluhu na Mwadui ya Shinyanga katika mchezo uliofanyika kwenye
Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kwa sare
hiyo, Yanga imeendelea kupiga kwata katika nafasi ya tano ya msimamo wa ligi
hiyo ikiwa na pointi 22, moja nyuma ya Singida United iliyopo katika nafasi ya
nne.
Simba na
Azam FC ambazo zinashika nafasi ya kwanza na pili kila moja ikiwa na pointi 26, kesho zina nafasi ya kuzidi kuikimbia Yanga endapo zitashinda mechi zao.
Simba
wanacheza dhidi ya Singida jijini Dar es Salaam wakati Azam FC watatoana jasho
dhidi ya Majimaji ya Songea mjini humo.
Katika
mchezo huo wa jana, Yanga nusura ipate bao katika dakika ya 23, kupitia kwa
Emmanuel Martin baada ya kuingia ndani ya 18, lakini kabla hajaleta madhara,
mabeki wa Mwadui walifanikiwa kumdhibiti.
Dakika ya
32, Amis Tambwe alipata nafasi nzuri ya kufunga, lakini alipiga mpira pembeni
kabla Paul Nonga hajashindwa kufunga katika dakika ya 33 baada ya kupiga shuti
lililodakwa na kipa wa Yanga, Youthe Rostand.
Mashabiki wa
Yanga hawakufurahishwa na matokeo hayo, ambapo baadhi yao walipiga kelele kuwa
hawamtaki kocha msaidizi wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa.
Nsajigwa
amekuwa akikaa katika benchi la timu hiyo baada ya kocha mkuu, George
Lwandamina wa Zambia kwenda kwao kwa ajili ya msiba wa mtoto wake.
Hata hivyo,
Lwandamina amesharejea nchini na jana alikuwepo jukwaani kwenye Uwanja wa Uhuru
wakati Yanga ikicheza na Mwadui.
Vikosi
vilikuwa Yanga: Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Andrew Vicent,
Kelvin Yondan, Said Juma, Juma Mahadhi, Pius Buswita, Amis Tambwe, Ibrahim
Ajibu na Emmanuel Martun.
Mwadui:
Anord Massawe, Jackson Salvatory, David Luhende, Joram Mgeveke, Idd Mfaume,
Awadhi Juma, Jean Girukwishako, Abdallah Omary, Paul Nonga, Evangestus Bernard
na Awese Awese.
No comments:
Post a Comment