TIMU ya Silabu FC ya Mtwara ambao ni mabingwa wa mkoa juzi wamenusurika
katika ajali iliyotokea Nchinga mkoani Lindi wakiwa safarini kwenda mkoa wa
Pwani kwa ajili ya mchezo wa kombe la Shirikisho la Azam ‘Azam Sports Federation’
Cup dhidi ya Kisarawe FC.
Akizungumza Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara, (MTWAREFA) Kizito Mbano alisema gari lililopata ajali ni
Coaster yenye namba T 159 DKQ ilikuwa imebeba watu 26, wachezaji 18, benchi la
ufundi watano na viongozi watatu.
“Basi aina ya Coaster ambayo ilikuwa inakwenda Pwani ilipata ajali eneo
la Nchinga, Lindi, watu 16 walipata majeraha na kukimbizwa katika hospitali ya mkoa
wa Lindi ya Sokoine baada ya gari kumshinda dereva nadhani alikuwa amelala
likayumba kushoto na kulia likaenda kugonga jiwe na kusimama,” alisema Mbano.
“Baada ya kupokelewa hospitali walipata matibabu lakini baada ya kuona
huduma ya hospitali ya Sokoine hairidhishi tuliomba kuondoka nao na majeruhi watatu ambao waliandikiwa kulazwa
na kuwapekeleka hospitali ya Ndanda ambayo ipo Masasi Mtwara,” aliongeza Mbano
Mbano aliwataja wachezaji waliolazwa ni Abdul Patrick ambaye anakohoa
damu, Karim Issa ameumia juu ya jicho na ana maumivu makali na Musa Musa ambaye
ana maumivu makali ya kichwa na wengine wanafanyiwa vipimo zaidi ili kujua kama
hawajaumia sana.
Akizungumza, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Alfred
Lucas alisema Rais Karia alisema TFF imepokea kwa masikitiko habari hiyo na
kuwaombea kwa Mungu ili wapone mapema.
“Mchezo huo umeharishwa hadi hapo baadae na Rais Karia anawaombea
majeruhi wapone haraka na kurejea katika afya ili waweze kuendelea na majukumu
yao ya kila siku,” alisema Lucas.
Azam
federation Cup ambayo inashirikisha timu 91 ambapo timu 16 ni za Ligi
Kuu, 24 za Ligi Daraja la Kwanza, 24 za Ligi Daraja la Pili na 27 za Ligi ya
Mabingwa wa Mkoa hatua ya awali ilianza kuchezwa Oktoba 31.
No comments:
Post a Comment