TAMBO zote za watani
wa jadi Yanga na Simba zimeisha kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Uhuru Dar
es Salaam leo.
Timu hizo ziliingia
uwanjani zikitoka kushinda mabao 4-0 katika mechi zao za mwisho, Yanga dhidi ya
Stand United Shinyanga na Simba dhidi ya Njombe Mji, Uhuru, matokeo ambayo
yalitoa hamu kushuhudia mechi yao ya jana kila mmoja akitaka kufahamu nani ni zaidi
ya mwingine.
Wakongwe hao walianza
mechi yao taratibu wakishambuliana kwa zamu na kumaliza kipindi cha kwanza
suluhu.
Simba ilipata bao la
kuongoza katika dakika ya 57 ambapo mchezaji wake Shiza Kichuya alifunga
akiunganisha pasi ya John Bocco aliyeingia dakika ya 56 kuchukua nafasi ya
Laudit Mavugo.
Bao hilo lilidumu kwa
dakika tatu tu kabla Obrey Chirwa hajaisawazishia Yanga akiunganisha pasi ya
Geofrey Mwashiuya.
Mechi ya jana haikuwa
na shangwe nyingi kama ilivyo kawaida ya mechi za watani pengine ni kutokana na
uchache wa watu waliofika uwanjani hapo kushudia mechi hiyo, tofauti na
ilivyozoeleka mechi hiyo hujaza mashabiki wengi.
Aidha, muda mwingi wa
mchezo wachezaji wa timu zote walionekana kucheza kwa kujilinda zaidi.
Dakika ya 22 Emmanuel
Okwi alipata nafasi nzuri ya kufunga lakini mpira wake wa kichwa ulitoka nje ya
goli.
Dakika moja baadaye
nusura Mwashiuya aipatie Yanga bao lakini mpira wake wa kichwa ulipaa nje.
Simba ilipata tena
nafasi katika dakika ya 27 ambapo mshambuliaji wake Mrundi Laudit Mavugo
alishindwa kufunga baada ya shuti lake kutoka pembeni ya goli.
Dakika ya 32 Chirwa
alikokota mpira mpaka kwenye boksi lakini akashindwa kufunga na mpira kupita
pembeni ya goli.
Sare hiyo inairudisha
Simba kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa uwiano mzuri wa mabao, huku Yanga
ikishika nafasi ya pili na Azam ya tatu. Zote zina pointi 16.
Yanga: Youthe
Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vicent, Kelvin Yondani, Papy
Tshitshimbi, Pius Buswita, Raphael Daud/ Pato Ngonyani, Obrey Chirwa,Ibrahim
Ajibu, Geofrey Mwashiuya/ Emmanuel Martin
Simba: Aishi Manula,
Erasto Nyoni, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jnr’, Juuko Murshid, Method Mwanjale,
James Kotei/ Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamiru Yassin/ Said Ndemla, Laudit
Mavugo/ John Bocco, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima.
No comments:
Post a Comment