MACHO na
masikio ya mashabiki wa soka leo yataelekezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar
es Salaam pale watani wa jadi, Yanga na Simba watakapomenyana katika mchezo wa
Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mashabiki wa
timu hizo wamekuwa wakitambiana kuanzia mitaani, nyumbani, katika vyombo vya
usafiri, sokoni, vijiweni na kila mahali, ambapo kila mmoja akitamba kuibuka na
ushindi leo.
UPINZANI MKALI
Upinzani
mkali kwa timu hizo unaonekana kuongezeka baada ya Yanga kumchukua mshambuliaji
hatari wa watani wao wa jadi Simba, Ibrahim Ajibu, huku Simba nao wakimchukua
Haruna Niyonzima.
Wawili hao
hasa Ajibu ameonesha makali na kuisaidia Yanga kupata mabao kibao, huku
mchezaji huyo naye akiwania kiatu cha dhahabu kama alivyo Emmanuel Okwi wa
Simba.
Ushindani
mkali utakuwa kwa Ajibu na Okwi katika mbio za kupachika mabao, kwani wachezaji
hao wameonesha makali yao karibu katika kila mchezo wa timu zao walizocheza.
Katika
msimamo wa ufungaji, Okwi anaongoza akiwa na mabao nane na amekuwa tegemeo
kubwa kwa timu yake ya Simba, hasa katika mechi zinazowakutanisha na Yanga,
kwani ana rekodi nzuri ya kuwafunga wapinzani hao.
Pia Okwi
amefunga katika michezo yote ya Ligi Kuu aliyocheza msimu huu hususani kwenye
Uwanja wa Uhuru, ambao ndio utakaotumika kuchezewa mchezo huo wa leo.
Ajib katika
msimamo wa ligi tayari ameshafunga mabao matano na ndiye mchezaji anayeongoza
kwa mabao kwa Yanga na hakuna ubishi kuwa mchezaji huyo yuko katika kiwango cha
juu cha uchezaji katika kipindi hiki huku akiwafunika Tambwe na Ngoma
Hivyo,
kulingana na ubora wa wachezaji hao wawili ni sababu mojawapo kubwa baina timu
hizi na wanatarajiwa kuwa nguzo katika mchezo huo wa aina yake na pengine kuwa
na upinzani wa juu zaidi.
Mchezo wa
watani wa jadi mara kadhaa wachezaji wanalaumiwa pindi timu moja inapopoteza
mchezo, makocha kufukuzwa pia viongozi hushambuliwa kwa maneno makali na mtaani
mashabiki wanataniana na ukiwa una hasira za karibu unaweza kujikuta unarusha
ngumi kwa sababu ya hizi timu mbili.
Katika
michezo saba iliyopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara zilizokutana tangu mwaka 2014
hadi 2017, Simba imeshinda michezo miwili na Yanga imeshinda miwili na kutoka
sare mitatu.
Matokeo ya mechi Yanga
na Simba
28/10/2017
Yanga ?? Simba
25/02/2017 Simba 2-1 Yanga
01/10/2016
Yanga 1-1 Simba
20/02/2016 Yanga 2-0 Simba
26/09/2015
Simba 0-2 Yanga
08/03/2015 Simba 1-0 Yanga
18/10/2014
Yanga 0-0 Simba
19/04/2014
Yanga 1-1 Simba
REKODI ZA MAKOCHA
Kwa
upande wa makocha, George Lwandamina hajawahi kuifunga Simba, hivyo rekodi inambeba Omog wa Simba ambaye
ameiongoza timu hiyo kuifunga Yanga katika mechi nne.
Mechi
ya kwanza Omog ilikuwa Oktoba mwaka jana katika mchezo wa Ligi Kuu, ambapo aliiongoza Simba kupata sare ya bao
1-1 licha ya timu yake kuwa pungufu uwanjani baada ya kiungo Jonas Mkude kupewa
kadi nyekundu na baadaye bao la kona ya winga Shiza Kichuya kumuokoa dakika za
majeruhi.
Mchezo
uliofuata wa Ligi Kuu ulikuwa Februari, ambapo aliibuka na ushindi wa mabao 2-1
licha ya timu yake kubaki tena pungufu uwanjani baada ya beki Besala Bokungu
kutolewa kwa kadi nyekundu.
Mechi
nyingine mbili alizocheza bila kufungwa na Yanga ni ule wa nusu fainali ya
Kombe la Mapinduzi aliposhinda kwa penalti 4-3 pamoja na mchezo wa Ngao ya
Jamii wa Agosti mwaka huu akishinda kwa penalti baada ya suluhu katika dakika
90.
Swali
linabaki Omog atafanikiwa kulinda rekodi yake mbele ya Yanga kwa kuibana na
kushinda au kutoa sare au atashindwa kulinda na kupokea kipigo kwa mara ya
kwanza tangu aanze kuinoa timu hiyo?
Katika
kujiandaa na mchezo huu timu zote ziliweka kambi nje ya Dar es Salaam wakati
Yanga wakiwa Morogoro, Simba ilipanda ndege hadi visiwa vya Zanzibar na wote
walitarajia kurejea jana tayari kwa mchezo huo.
Tusubiri
baada ya dakika 90 nini kitatokea katika mchezo huo maarufu kama Kariakoo `Derby’ ambayo
ni miongoni mwa mechi kubwa tatu barani Afrika baada ya ‘Cairo Derby’ ambayo
huzihusisha timu pinzani nchini Misri, Al Ahly dhidi ya Zamalek na ‘Soweto
Derby’ inayohusisha timu za Orlando Pirates dhidi ya Kaizer Chiefs zote
za Afrika Kusini.
MAKOCHA KUTIMULIWA
Mechi za Yanga na Simba
zimekuwa balaa kwa makocha, kwani wakati mwingine wanajikuta wakitimuliwa
kutokana na matokeo ya uwanjani kutokuwa mazuri kwa timu zao.
Hata hivyo, katika mchezo
wa leo, Omog ndiye anayeonekana kuwa katika hatari zaidi ya kutupiwa virago
endapo atafungwa, kwani tayari uongozi wa timu hiyo ulishawahi kumchimba mkwara
kwa matokeo mabaya ya nyuma.
Kocha Omog pamoja na
kukibadilisha kikosi chake na kucheza kandanda safi bado uongozi unaonesha
wakati fulani kutoridhika na matokeo hayo.
Kwa upande wa Mzambia
George Lwandamina wa Yanga, yeye anaonekana hayuko hatari sana kwani Yanga
wameonesha kumkubali na hivyo wako tayari kumvumilia aendelee kuwepo katika
kikosi chao.
Hata hivyo, uongozi na
mashabiki wa timu hizo mbili huwa hawana msamaha pale wanapoona timu yao
imefanywa 'kitu mbaya' na wapinzani wao wa jadi na kuwakosesha usingizi.
No comments:
Post a Comment