MWAMUZI wa
Tanzania Israel Nkongo anatarajiwa kuchezesha mchezo wa kihistoria wa kirafiki
kati ya Everton ya England dhidi ya Gor Mahia kutoka Kenya utakaofanyika keshokutwa
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Nkongo
ambaye ana beji ya FIFA, atasaidiwa na Ferdinand Chacha, Frank Komba na mezani
atakuwa ni Hery Sasii na Kamishna wa mchezo ni Michael Wambura.
Akizungumza
na wandishi wa habari jana Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa ambao ndio waratibu
wa mchezo huo Abass Tarimba alisema maandalizi ya mechi yamekamilika na kinachosubiriwa
ni timu hizo kuwasili.
“Maandalizi yamekamilika
hivyo niwaombe mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwaona wachezaji wanasifika
kwenye Ligi Kuu ya England kwani Rooney atakuja na amekuwa na hamu ya kufika
baada ya kusikia magwiji kandaa wametembelea Tanzania,” alisema Tarimba.
Naye Meneja
Miradi wa Selcom ambao ndio wanauza tiketi za mchezo huo Gallus Runyeta alisema
zoezi la uuzaji tiketi linaendelea na mtu asiye na kadi anaweza kuwahi mapema
siku ya mchezo kwani zitakuwepo uwanjani.
“Mtu mmoja
anaweza kununua tiketi yake na kumnunulia mtu mwingine ambaye ana kadi hivyo
nawaomba mashabiki wajinunulie tiketi mapema,” alisema Runyeta.
Naye Ofisa
Usalama wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), Inspekta Hashim Abdallah
amewataka mashabiki watakaojitokeza kwenye mchezo huo kuachana na mahaba kwa
wachezaji ikiwemo kwenda kuwakumbatia kwani hawataruhusiwa kufanya.
“Mshambuliaji
Wayne Rooney atakuwepo kwenye msafara huo, kuna watu watataka kwenda kumkubatia
hawataruhusiwa kwani itasababisha usumbufu,” alisema Hashim.
Viingilio
katika mchezo huo ni shilingi 8000 kwa VIP B na C na mzunguko ni sh 3000 wakati
VIP A itakuwa maalum kwa watu mashuhuri.
Gor Mahia ambayo
kwa sasa inanolewa na Dylan Kerraliyewahi kufundisha Simba waliwasili jana mchana
na Everton wanatarajiwa kuwasili leo asubuhi na baada ya kuwasili watafanya
shughuli mbalimbali za kijamii.
Baada ya
kuwasili Everton itafanya kliniki ya soka na kuzuru sehemu mbalimbali kuanzia
saa 5:30 hadi saa 11:00 kwani wataanza kutoa huduma shule ya msingi ya Uhuru
Kariakoo, klabu ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Sea Cliff na Gymkana
Kwa upande
wa Gor Mahia saa 9:00 alasiri mpaka saa 10:00 jioni watakuwa Uwanja wa Taifa
kwa ajili ya mkutano na wandishi wa habari baadae watakuwa Uwanja wa Uhuru wakifanya
mazoezi hadi saa 12:00 jioni.
Everton watafanya
mkutano na waandishi wa habari saa 10:30 jioni mpaka 11:00 jioni Uwanja wa
Taifa na saa 11:00 jioni mpaka saa 1:30 usiku watafanya mazoezi katika Uwanja wa
Taifa.
Keshokutwa kuanzia
saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana wawakilishi wa timu zote watatembelea
hospitali ya Pugu Kajiungeni na watazuru Maasai Cultural Center kujionea tamaduni
mbalimbali za kabila hilo.
Mchezo
utaanza kuchezwa saa 11:00 jioni na milango ya uwanjani itaanza kufunguliwa
kuanzia saa nne asubuhi ili kutoa fursa ya watu kuingia kwa muda muafaka bila
bughudha.
No comments:
Post a Comment