YAMETOLEWA
maoni tofauti baada ya uamuzi wa kubaki klabuni Arsenal kwa kocha wao, Arsene
Wenger, baada ya msimu uliowatupa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa mara
ya kwanza tangu miongo miwili.
Wakati
wachezaji kadhaa wa zamani wa Arsenal kama Ian Wright na David Seaman wakiona
kwamba kuondoka kwa Mfaransa huyo kingekuwa kiama kwa timu, wapo wengine
wanaosema kumbakisha ni sawa na kufurahia njaa na kuifanya iwe endelevu.
Mchambuzi wa
masuala ya soka, Gary Lineker anadai kwamba Wenger anajiona kwamba amefanikiwa
sana Arsenal, lakini ukweli ni kwamba yupo nyuma sana akilinganishwa na
wapinzani wake wakubwa kwenye Ligi Kuu ya England (EPL).
Lineker
ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa England anakwenda mbali zaidi akionesha
uchuro, ambapo anasema uwezekano mkubwa ni kushindwa tena kufuzu kwa UCL msimu
ujao kwa sababu hawezi kupata wachezaji matata kuliko klabu nne zilizo juu yake
na pia baadhi za chini, kama Manchester United.
Wenger
amekubali mwito wa mmiliki wa klabu hiyo, Stan Kroenke, na kusaini mkataba mpya
wa miaka miwili kuanzia kiangazi hiki, wakati baadhi ya washabiki na wadau wa
Arsenal walitaka mabadiliko kwa kuwa na kocha mpya wakati huu.
Lineker
anaungwa mkono na golikipa wa zamani wa Arsenal, Bob Wilson anayesema
anachokiona ni ugumu kwa klabu hiyo ya London Kaskazini kuvutia wachezaji wa
hadhi ya juu.
“Unawezaje,
kwa mfano kumpata mtu kama Antoine Greizmann aje hapo kusaini mkataba? Bila
kuwa kwenye michuano ya UCL njia pekee unayoweza kuwavutia wachezaji wakubwa ni
kuwalipa mishahara mikubwa,” anasema, ikijulikana jinsi Wenger asivyopenda
kutoa mishahara minono.
Anatoa mfano
wa Chelsea walivyomsajili N’Golo Kante kiangazi kilichopita licha ya kumaliza
chini ya Arsenal, huku The Gunners nao wakitaka kumsajili kutoka Leicester
lakini akakataa kwa sababu ofa yao ya mshahara ilikuwa chini sana na hata
wakiwa UCL kwake haikuwa na maana.
“Bodi ya
Wakurugenzi ya Arsenal ilitakiwa kutazama mambo katika uhalisia wake, ijiulize
iwapo katika mazingira haya watashindana kweli? Hawawezi kuchuana na Manchester
City wala Chelsea kwa fedha yote ambayo Roman Abramovich na Sheikh Mansour
walizo nazo na wanazolenga kuwekeza kwenye klabu zao.
Wachambuzi
wanajiuliza iwapo Wenger anaweza tena kwa sasa kuleta mabadiliko Arsenal, akiwa
amekaa kwa miaka 21, akawa na wachezaji tofauti 162 katika muda huo na kutumia
pauni milioni 700 kwao. Lineker anasema Arsenal wapo nyuma kuliko Wenger
anavyodhani na daima akiwa hapo atakuwa chini ya shinikizo.
Kroenke
alikutana na Wenger Jumatatu, wakakubaliana mambo kisha uamuzi huo ukapelekwa
kwenye Bodi ya Wakurugenzi, kama kutimiza tu wajibu, kwa sababu Kroenke mwenye
hisa asilimia takriban 70 ndiye mwenye usemi na anayemfuatia, Alisher Usmanov
amefungiwa nje ya bodi hiyo.
Hata hivyo,
Kocha wa cheslea, Antonio Conte amemtaja Wenger kuwa kocha bora zaidi katika
historia hapo.
No comments:
Post a Comment